Yowe ya kuvamiwa na wanyonya damu ,
iliyopigwa na wanawake waliokuwa wakichimba chumvi katika Kijiji cha
Iringa-Mvumi wilayani Chamwino, Mkoa wa Dodoma ndiyo iliyosababisha kuuawa kwa
watafiti wa Chuo cha Utafiti wa Udongo na Maendeleo ya Ardhi cha Selian mkoani
Arusha.
Watafiti hao waliuawa juzi kwa
kukatwa katwa mapanga na minde, kisha kuchomwa moto. Gari la Serikali aina ya
Toyota Hillux, pia lilichomwa moto.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma,
Lazaro Mambosasa alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba wanawashikilia
watu kadhaa akiwamo mwenyekiti wa kijiji.
Alisema mwenyekiti wa kitongoji
alipigiwa simu na mmoja wa wanawake waliokuwa eneo la tukio kwamba kuna
wanyonya damu wamevamia kijiji.
Mambosasa alisema kwa kuwa
mwenyekiti huyo alikuwa mbali, alimpigia simu mwenyekiti wa kijiji aende eneo
la tukio kujua kilichotokea. Alisema mwenyekiti wa kijiji alipofika hakuamini
maelezo ya watafiti hao na kuanza kuwashambulia.
Mambosasa alisema mtu mwingine
alikwenda kijijini na kumueleza mchungaji wa kanisa kuhusu kijiji kuvamiwa na
nyonya damu, naye akatagaza kwenye kipaza sauti kwamba kijiji kimevamia na watu
hao.
Alisema wanakijiji walijitokeza
kwenda eneo la tukio na kuwashambulia watafiti hao hadi kufa.
Mkuu wa Mkoa, Jordan Rugimbana
alisema baada ya kutembelea eneo la tukio, ameamua kuwasimamisha kazi kaimu
mkurugenzi wa halmashauri ya Chamwino na ofisa utumishi wa wilaya hiyo kwa
madai ya kutosambaza barua za kuwatambulisha watafiti hao katika maeneo
waliyokwenda kufanya kazi.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo,
Simon Kawea alisema taarifa alizozipata kutoka kwa diwani wa kata ya
Iringa-Mvumi, watafiti hao walipofika katika eneo la Makamwa walikutana na watu
na kuwauliza kilipo kijiji cha Iringa-Mvumi.
Kawea alisema watafiti hao
walipofika eneo walilotaka kufanya utafiti walipigiwa yowe kwamba ni wanyonya
damu.
Alisema baada ya kelele zile
wanakijiji waliokuwa katika mkutano walisikia na kutoka na mapanga na silaha za
jadi kisha kuwavamia watafiti hao na kuwashambulia kwa silaha hizo.
“Hata walipoonyesha vielelezo wao
si wezi bali ni watafiti waliopewa kibali na halmashauri ya Chamwino na
vielelezo vingine, wanakijiji walikataa na kuendelea kuwapiga,” alisema.
Alisema watendaji wa kijiji hicho
na diwani wa kata hiyo, Robert Chikole waliwasihi wanakijiji kuwaacha watafiti
hao lakini walizidiwa nguvu na wananchi.
Aliongeza: “Hata polisi
walifika muda mfupi, walikuta wameumizwa vibaya wakarusha risasi juu lakini
walizidiwa nguvu na kukaa pembeni. Kwa kweli wamekufa katika tukio la kinyama,” alisema.
Alisema watafiti hao walikwenda
katika ofisi za Wilaya ya Chamwino na kupata kibali kabla ya kwenda kijijini
hapo kwa ajili ya kufanya utafiti wa udongo.
Alisema diwani, mtendaji na
mwenyekiti wa kijiji wanashikiliwa na polisi kuhusiana na tukio hilo.
Habari kutoka kijijini hapo
zinasema wanakijiji wamekimbia makazi yao kutokana na msako wa polisi kwenye
eneo hilo.
Majonzi yatawala Arusha
Mauaji ya hayo yameibua simanzi
katika taasisi ya Selian na familia zao, ikiwamo ya mkurugenzi wa taasisi hiyo,
Dk January Mfuru ambaye mtoto wake pia ameuawa.
Mtoto huyo, Faraji Mafuru amehitimu
Chuo cha Mipango Dodoma hivi karibuni na alikuwa katika mazoezi kwa vitendo.
Mratibu wa utafiti katika kituo
hicho, Dk Charles Lyamchai alisema tukio hilo limetokea wakati timu ya watafiti
wa kituo hicho ikiwa mkoani Dodoma kutekeleza mradi wa kukusanya sampuli za
udongo kwa ajili ya kuziingiza kwenye kanzidata ya Taifa.
“Hawa walikuwa kwenye mradi maalumu
ambao umeanza mwaka 2014 na wapo wengine watafiti ambao wamesambaa kwenda
mkoani Dodoma kwa kazi hii,” alisema.
Aliwataja wengine waliouawa kuwa ni
dereva Nicas Magazine na Mtafiti wa maabara ya udongo, Teddy Lumanga.
“Wapo watumishi 10 huko kutoka hapa
kituoni, waliokwenda kutekeleza mradi wa kutambua kiwango cha rutuba kwenye
udongo nchini ambao tumeshaukamilisha kwenye wilaya zote za mikoa ya Kanda ya
Kaskazini na Katavi na wilaya ya Kondoa, hili ni jambo la kushtua sana,”alisema.
Alisema watafiti hao walikuwa
katika wiki ya pili na hawakuwa wamepata matatizo yeyote tangu wafike Dodoma,
baada ya tukio hilo kiongozi wa msafara aliwasiliana na kituo.
Dk Lyamchai alisema kabla ya
kwenda huwa wanatoa taarifa kwa kuandika barua kwenye wilaya husika, pia maeneo
ya vijijini huwa wanaambatana na mabwana shamba.
“Watafiti wetu hawana mahusiano
yoyote na masuala ya damu, walikuwa kwenye kazi zao na walitoa taarifa hadi
ofisi ya kata ila hatujui ni kwa nini tukio hili limejitokeza,” alisema.
Mtafiti mwandamizi wa kituo hicho,
Dk Lameck Makoye alisema hawajawahi kukutana na changamoto kubwa kama hiyo hasa
maeneo ambayo huwa na historia ya wenyeji wasiopenda wageni.
Alisema Dk Mafuru na watafiti
wengine waliondoka jana kwendas Dodoma kuungana na watafiti wengine kutoka
Kituo cha Hombolo na Makutupola kwenda eneo la tukio.
Selian ni miongoni mwa vituo
maarufu katika Ukanda wa Afrika ya Mashariki na Kati kwa kufanya tafiti za
mazao katika maeneo yenye ukame nchini.
No comments:
Post a Comment