Chama cha ACT- Wazalendo kimepanga
kuwasha moto mjadala wa Katiba mpya katika mkutano wake kidemokrasia kilioitisha
jijini Dar es Salaam Oktoba 8.
Mkutano huo unalenga kufufua
mchakato wa Katiba Mpya kwa kuzingatia michakato ya katiba za nchi nyingine za
Afrika, alisema Katibu wa itikadi na uenezi wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu
alipozungumza na waandishi jijini Dar es Salaam jana.
Alisema katika kupata uzoefu, ACT
Wazalendo imemualika Adabu Namwamba, ambaye ni kiongozi wa Chama cha Labour cha
Kenya kilichofanikiwa kubadilisha katiba yake baada ya mchakato mrefu.
Aliwataja wageni wengine kuwa
ni mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania, Deus Kibamba ambaye naye atatoa
mada kuhusu suala hilo.
Mchakato wa kuandika Katiba mpya
nchini umekwama katika hatua ya kupiga Kura ya Maoni baada ya Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC) kushindwa kukamilisha uandikishaji wapigakura kwa muda
uliotakiwa.
Mchakato huo uligubikwa na vikwazo
kadhaa, ikiwa ni pamoja na vyama vinne vya upinzani na baadhi ya wajumbe
kususia kwa maelezo kuwa Bunge liliacha Rasimu ya Katiba iliyokuwa na maoni ya
wananchi na kuingiza sera za CCM.
Katika mkutano huo, kiongozi wa ACT
Wazalendo, Zitto Kabwe atawasilisha mada kuhusu hali ya nchi kwa mtazamo wa
chama hicho.
“Kiongozi wetu atawasilisha
uchambuzi mpana wa kina zaidi kuhusu hali ya nchi yetu kiuchumi, kisiasa na
kijamii tangu Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani,” alisema.
Pia, mwenyekiti wa ACT Wazalendo,
Anna Mghwira, ambaye aligombea urais mwaka jana, ataeleza uzoefu wake katika
uchaguzi, wakati mshauri wa chama hicho, Profesa Kitila Mkumbo atachambua
mwelekeo wa chama hadi mwaka 2020.
“Chama kinatoa wito kwa wananchi
wanaotaka kushiriki katika mkutano huo kuwasiliana na ofisi ili kujiandikisha,” alisema.
No comments:
Post a Comment