WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
ameagiza apatiwe orodha ya wadaiwa sugu wa taasisi zote za Serikali mkoani
Dodoma ambao wamelimbikiza deni la sh. bilioni 1.4 zikiwa ni bili zao za maji.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo
Jumapili, Oktoba 2, 2016 wakati akizungumza na watumishi na viongozi wa Mamlaka
ya Maji Safi na Maji Taka Dodoma (DUWASA) mara baada ya kukagua utendaji kazi
wa chanzo cha maji cha Mzakwe nje kidogo ya mji wa Dodoma.
“Niletee haraka orodha ya wadaiwa
wote wa Ofisi za Serikali na taasisi za umma ambao hawajalipa bili zao. Madeni
yote ni lazima yalipwe,” amesema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu ambaye yuko katika
ziara ya siku mbili ya kukagua maandalizi ya Serikali kuhamia Dodoma,
anatembelea sehemu mbalimbali za kutolea huduma za jamii pamoja na kukagua
miundombinu ya mkoa huo.
Aliutaka uongozi wa DUWASA na
watumishi wote wahakakishe wanaboresha huduma za upatikanaji wa maji hasa
kwenye maeneo yanayopimwa viwanja ili wananchi au wawekezaji wanaponunua
viwanja wakute huduma hiyo ipo na waanze ujenzi mara moja.
“Tumealika wawekezaji, nataka
wajenge viwanda na mahoteli hapa Dodoma, sasa wakikuta maji na umeme kwenye
maeneo yao, itakuwa ni kichocheo cha kuharakisha kazi za ujenzi,” amesema.
Pia amemwagiza Mkuu wa Wilaya ya
Dodoma, Bi. Christina Mndeme ahakikishe eneo lililo jirani na chanzo hicho cha
maji halikaliwi na mtu yeyote na linalindwa dhidi ya uchomaji mioto.
“Uchomaji moto uoto wa asili
umeharibu vyanzo vingi vya maji. Ni tatizo kubwa hapa nchini na halina budi
kusimamiwa hadi liishe,” amesisistiza.
Amefikia uamuzi huo baada ya
kupokea taarifa kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Mhandisi David
Pallangyo kwamba kuna wananchi wameanza kujenga na kufanya shughuli za kijamii
jirani na chanzo hicho licha ya kuwa walikwishaondolewa zamani.
Kuhusu wadaiwa sugu, Mhandisi
Pallangyo alisema mashirika ya umma na taasisi za Serikali ndiyo wanaongoza kwa
kulimbikiza madeni. “Wananchi wa kawaida wapo wanaodaiwa lakini deni lao siyo
kubwa na hao tunawamudu,” alisema wakati akizungumza na mwandishi wa habari
hizi.
Alisema changamoto nyingine
inayowakabili ni uchomaji moto ambapo hivi karibuni uliwashwa moto na kuunguza
baadhi ya nguzo za umeme ambazo zinapeleka umeme kwenye chanzo hicho.
Alisema askari wa JKT Makutupora
walisaidia kuzima moto huo ili usifike kwenye mitambo mingine ya chanzo hicho
cha maji.
Waziri Mkuu pia alikagua maabara ya
upimaji maji kwenye chanzo hicho kabla hayajasambazwa kwa wateja na mara yanapokuwa
yamefika kwa wateja na kuelezwa kuwa maji hayo yanakidhi viwango vya kitaifa na
vya kimataifa vilivyowekwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Waziri Mkuu anaendelea na ziara
yake kwa kutembelea kiwanda cha magodoro Dodoma na kituo cha kuzalisha umeme
cha Zuzu.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI
MKUU
JUMAPILI, OKTOBA
2, 2016
No comments:
Post a Comment