Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC) Jaji Mstaafu Damian Lubuva amesema kuwa Tume ya Taifa ya
Uchaguzi itaendelea kutoa elimu ya Mpiga Kura kote nchini ili kuwajengea
wananchi uelewa sahihi juu majukumu ya Tume na chaguzi zinazofanyika
nchini.
Akizungumza jijini Dar es Salaam
Jaji Lubuva amesema baadhi ya wananchi wamekuwa wakishindwa kutimiza Haki yao
ya Kikatiba ya kupiga Kura kuwachagua viongozi wananowapenda kwa sababu ya
kukosa uelewa juu ya Sheria, Kanuni na taratibu zinazosimamia Uchaguzi .
Amesema Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania 1977 inaipa NEC jukumu la kusimamia na kuendesha Uchaguzi
wa Rais, Wabunge na Madiwani kwa upande wa Tanzania Bara na kubainisha
kuwa ili jukumu hilo lifanywe kwa ufanisi wananchi waliotimiza vigezo vya
kupiga kura na wale wanaotarajia kupiga kura miaka ijayo lazima
wapatiwe elimu sahihi ya Mpiga Kura.
Amefafanua kuwa baada ya kumalizika
kwa Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani mwaka 2015, NEC ilianza
kutekeleza programu mbalimbali ikiwemo kutoa elimu ya Mpiga Kura kuwafikia
wananchi moja kwa moja kupitia mikutano mikubwa inayohusisha viongozi mbalimbali,
maonesho ya Sabasaba na Nane Nane , kutoa elimu ya Mpiga kura kwenye
vyombo mbalimbali vya habari pamoja na kuzitembelea baadhi ya shule za
Sekondari za mkoa wa Singida na Mara.
” Moja ya shughuli za Tume ni
kuendesha na kusimamia uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani nchi nzima kwa
upande wa Tanzania Bara, ili shughuli hii tuifanye vizuri ni muhimu sana
tuwapatie wananchi elimu sahihi juu ya upigaji wa kura, tutafanya jambo hili
tukishirikiana na wadau na Asasi nyingine ambazo tutazipa kibali cha
kutoa elimu hii”Amesisitiza Jaji Lubuva.
Jaji Lubuva amebainisha kwamba
utoaji wa elimu hiyo utaongeza idadi ya wapiga kura kwenye chaguzi zijazo
akitoa mfano wa idadi pungufu ya wapiga waliojitokeza kwenye Uchaguzi Mkuu wa
mwaka 2010 na ule uliofanyika Oktoba 25 , 2015 ambapo baadhi ya wananchi
walioandikishwa kwenye daftari la kudumu la Wapiga Kura na kupewa vitambulisho
hawakujitokeza kupiga kura.
” Tunalenga kuongeza uelewa wa
wananchi kuhusu majukumu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi pia umuhimu wa wananchi
kushiriki Kupiga Kura, baadhi ya wananchi wamekuwa wakijitokeza ili wapate
vitambulisho jambo ambalo sio sahihi, mfano mwaka 2010 wananchi milioni
15 walijiandikisha kupiga kura lakini waliojitokeza kupiga kura ni milioni
8.626 hii ni idadi ya chini, pia mwaka 2015 wananchi waliojiandikisha
walikuwa milioni 23,161,440 lakini waliojitokeza Kupiga Kura ni watu milioni
15,589,639 hapa kuna ongezeko, tunaamini tukiwapatia elimu wengi zaidi
watajitokeza kuwachagua viongozi wanaowapenda ”Amesitiza Jaji
Lubuva.
Amesema katika kuendelea kupanua
wigo wa utoaji wa elimu ya Mpiga Kura kwa wananchi wengi zaidi NEC itashiriki
Kongamano na maonesho ya Wiki ya Vijana yatakayoambatana na Maadhimisho ya
Kumbukumbu ya Baba wa Taifa na Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru 2016 Oktoba 7
hadi 14, 2016 mkoani Simiyu ambapo pamoja na Mambo mengine watendaji na Maafisa
wa Tume watatoa elimu ya Mpiga Kura kwa wananchi na kutembelea shule za
Sekondari za mkoa huo.
Aidha, ili kuboresha chaguzi zijazo
ametoa wito kwa wananchi waendelee kushirikiana na Tume kwa kujitokeza
kwa wingi kuuliza maswali na kupata ufafanuzi wa hoja mbalimbali katika maeneo
ambayo watendaji wa NEC watafika kutoa elimu ya Mpiga Kura.
Na Aron Msigwa – NEC
No comments:
Post a Comment