Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO,
Dodoma
Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
imejipanga kuhamishia Bodi ya Pamba katika Mkoa wa Mwanza kabla ya Novemba 10
mwaka huu ili kuhakikisha wakulima wa pamba waliopo katika mkoa huo wanapata
huduma zilizo bora kwa ukaribu na haraka.
Hayo yamesemwa jana mjini Dodoma na
Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. William Ole Nasha alipokuwa akijibu
swali la Mbunge wa Bukombe Mhe. Doto Biteko lililohoji juu ya hatua ya Serikali
kwa wakulima walioathirika na pembejeo zilizotolewa ambazo hazikuwa na ubora
pamoja na kuhamishia Bodi ya Pamba katika mkoa huo.
”ili kuwafikia kirahisi wakulima wa
pamba waliopo mkoani Mwanza, Wizara imeamua kuhamishia Bodi hiyo katika mkoa
huo na kwa taarifa zilizopo Bodi hiyo inatakiwa kuhama haraka iwezekanavyo
kabla ya Novemba 10 mwaka huu”, alisema Mhe.Ole Nasha.
Kwa upande wa matatizo ya pembejeo,
Mhe. Ole Nasha alisema kuwa Serikali tayari ina taarifa kuhusu tatizo
lililowapata wakulima wa pamba katika maeneo mbalimbali kwa kusambaziwa
viuatilifu pamoja na mbegu ambazo hazikuwa na ubora unaotakiwa hivyo kuathiri
wakulima nchini.
“Serikali iliiagiza Tropical
Pesticides Research Institute (TPRI) kufanya uchunguzi wa malalamiko ya
wakulima ambao ulibaini kuwa viuatilifu hivyo vilikuwa na utendaji hafifu hivyo
Serikali itaanza kuzalisha mbegu bora za pamba za UK08 ili kuhakikisha tatizo
hili halijirudii tena”, alisema Mhe. Ole Nasha.
Naibu Waziri huyo amefafanua kuwa
kufuatia changamoto hizo za uotaji wa mbegu, Serikali iliamua kufanya majaribio
ya utoaji wa mbegu ambazo zilikuwa zikisambazwa hapo awali bila kujua ufanisi
katika uotaji wake.
Alithibitisha kuwa, matokeo ya
jaribio hilo yamewezesha kutoa maelekezo kuhusu aina za mbegu za pamba zenye
sifa za msingi ambazo zitasambazwa kwa wakulima katika msimu wa kilimo wa mwaka
2016/2017.
No comments:
Post a Comment