Gazeti la Tanzania Daima limeripoti
kuwa Serikali imeanza uhakiki wa vyeti vya ndoa kwa watumishi wa umma. Hatua
hiyo ambayo imewashtua watumishi wengi wa umma, imeelezwa kuwa ni mwendelezo wa
harakati za Serikali ya Rais John Magufuli kuhakiki watumishi wa umma ili
kuondokana na watumishi hewa.
Wakati Serikali ikianza na uhakiki
wa vyeti vya ndoa, kazi ya uhakiki wa watumishi hewa na vyeti vyao vya elimu
inaendelea sehemu mbalimbali nchini.
Kwa muhibu wa Gazeti hilo, habari
ambazo limezipata zinasema kuwa serikali imeanzisha uhakiki huo nchi nzima kwa
madai kuwa baadhi ya watumishi wa umma wamekuwa wakitoa taarifa za uongo kwamba
wana ndoa ili kupata nauli na stahiki zingine za likizo wakati hawana ndoa.
Habari zaidi zinasema kuwa walimu
wakuu wa shule zote za Wilaya ya Ilala wamepewa siku mbili kutekeleza agizo
hilo kwa walimu wao.
Mmoja wa walimu hao ambaye ameomba
jina lake lihifadhiwe, alilithibitishia Tanzania daima kuwa ametoa siku
mbili kwa walimu wa shule yake wenye vyeti vya ndoa waviwasilishe kwake.
"Kweli tumepewa agizo hilo leo
manispaa ya Ilala na tumetakiwa kuwasilisha vyeti hivyo kesho na tayari baadhi
ya walimu wangu wamefanya hivyo leo na kesho zoezi hilo linakamilika"
Alipoulizwa sababu ya kuwepo kwa
zoezi hilo, mwalimu huyo alisema hajui lakini anahisi lina lengo la kudhibiti
taarifa za uongo za watumishi wakati wa kuomba likizo.
Wakati walimu wa shule za Ilala
wakitakiwa kuwasilisha vyeti vyao vya ndoa, wilaya nyingine za Temeke,
Kinondoni, Ubungo na Kigamboni hawana taarifa hizo.
Mmoja wa walimu kutoka Manispaa ya
Ilala alisema kuwa uhakiki huo una lengo la kutaka kuchelewesha zaidi malipo na
stahiki za walimu za likizo ambazo hazijalipwa kwa miaka mingi.
No comments:
Post a Comment