Mbunge wa Kigoma Mjini Zitto Kabwe
amemshauri Rais wa Tanzania Dkt. John Magufuli kulivunja Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania endapo analiona ni kikwazo kwake.
Ushauri huo ameutoa jana ikiwa ni
saa chache baada ya Rais Magufuli kukosoa uamuzi wa Bunge kumuita Mkuu wa Mkoa
wa Dar es Salaam Paul Makonda kujieleza mbele ya Kamati ya Bunge, kutokana na
kilichodaiwa na wabunge kuwa ni kauli ya kulidhalilisha Bunge.
Katika hotuba yake aliyoitoa jana
wakati wa kuapishwa kwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa
za Kulevya, Rais Magufuli aliwataka viongozi wengine kumuunga mkono mtu
anayejitokeza kupiga vita dawa za kulevya badala ya kumdhalilisha.
"Tunapomuona mtu anajitokeza
kupambana na haya madawa ya kulevya, badala ya kumdhalilisha tumuombee na
kumtia moyo, hawa wanaweza hata kubadilisha maneno uliyoyazungumza
wakabadilisha wakatengeneza kwenye clip wakatupa, na wakajitokeza wengine
wakasema wameingilia mamlaka yao, wakati wao wanaingilia mamlaka ya kuwaita
wengine, hii ni vita". Alisema Magufuli
Baada ya kauli hiyo ya Rais, Zitto
kupitia ukurasa wake wa Facebook ameonesha kushangazwa na kile alichodai
kuwa Rais hakujua kuwa sheria ya kuundwa kwa mamlaka hiyo, ilitungwa, na kwamba
anashangaa kuona Rais hakuwa akijua kuwa alipaswa kumteua Kamishna Mkuu wa
Mamlaka hiyo
Ujumbe wa Zitto unasema
"Wabunge walitoa Hoja Binafsi
kuhusu Madawa ya kulevya ( Esther Bulaya na Faustine Ndugulile ) na kufuatia
hoja hiyo Serikali ikaleta Muswada bungeni na Bunge likatunga Sheria ya
Kupambana na Madawa ya kulevya mwaka 2015.
"Serikali mpya ikaingia
madarakani mwezi Novemba 2015. February 2017 Ndio Kamishna Mkuu anateuliwa tena
baada ya wabunge kuhoji na kushinikiza kupitia Kamati husika na pia mbunge
Esther Bulaya aliyetoa Hoja Binafsi katika Bunge la Kumi.
"Rais anasema hakuwa anajua
kuwa sheria hiyo ipo. Lakini Rais anapogawa Wizara huwa anatoa instruments na
Hizo instruments hutaja kila sheria kwa kila Waziri. Ilikuwaje Rais akasahau
sheria hii nyeti kama alikuwa na nia ya dhati ya Kupambana na Madawa ya
kulevya?
Rais anaona Bunge kikwazo kwa
sababu Bunge linamwongoza afuate sheria. Lakini Kama anaona Bunge linamkera
turudi kwenye uchaguzi tu, alivunje".
No comments:
Post a Comment