Watu wanne wamepoteza maisha na wengine watatu kujeruhiwa baada
ya kufukiwa na kifusi katika machimbo ya Nyamalinde kijiji cha Sobola nje
kidogo ya wilaya ya Geita, mkoani Geita.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo amesema
tukio hilo limetokea jana majira ya saa mbili asubuhi katika machimbo
hayo yanayomilikiwa na wananchi licha ya kuwa tayari yalishapigwa marufuku
kuendelea kwa kazi hiyo.
Mponjoli amesema tukio hilo limetokea baada ya watu 7 kuingia
ndani ya mgodi huo, lakini muda mfupi baadaye kifusi kikawaangukia na
kusababisha vifo vya watu wanne kati yao huku watatu wakitoka salama licha ya
kuwa na majeraha.
Amewataja watu waliopoteza maisha kuwa ni pamoja na Robert
Kazegemwa, Jeremia Emmanuel, Makenya Mwita na Julius Timotheo.
Waliojeruhiwa ni pamoja na Mashaka Samuel, Justine Safari na
Maneno Lusika ambao wanapatiwa matibabu katika hospitali ya Katoro.
Katika tukio lingine, jana majira ya saa 7 mchana tetemeko dogo
la ardhi limetikisa katika mkoa wa Geita ambapo licha ya kutokuwa na madhara
yoyote, limezua taharuki katika maeneo mbalimbali ikiwemo katika shule ya
sekondari Nyang'wale.
Kamanda Mponjoli amesema katika shule hiyo, wanafunzi walikuwa
katika mitihani na ndipo walipokimbia kutoka darasani ili kujiokoa ambapo
kutokana na msukumano, mwanafunzi mmoja alijeruhiwa lakini tayari
amekwishapatiwa matibabu na yuko salama
No comments:
Post a Comment