Mbunge wa viti maalumu (CCM), Jackline Ngonyani jana alizua kizaazaa bungeni baada ya kuwaambia wabunge wa upinzani wamekosa dira kiasi cha kula rambirambi zilizotolewa kwenye msiba wa Philemon Ndesamburo.
Alitoa kauli hiyo alipokuwa akichangia mjadala wa bajeti ya mwaka 2017/18. Baada ya kuzungumzia hoja zake, Ngonyani alielezea kilichotokea kwenye salamu za pole zilizotolewa wakati wa msiba wa muasisi huyo wa Chadema aliyewahi pia kuwa mbunge wa Moshi Mjini kwa vipindi vitatu mfululizo.
Mbunge huyo alianza kwa kumpongeza Rais John Magufuli kwa utekelezaji wa ilani ya CCM na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambayo inawagusa wananchi, akidai utekelezaji huo unawanyima hoja wapinzani.
Aliyafananisha maneno ya wapinzani na miti kuteleza siku ya kifo cha nyani, akisema licha ya kueleza kwamba Rais anatumia sera zao, wapinzani hao wamesahau changamoto zinazowakabili wananchi kwenye majimbo yao.
Mbunge huyo alimshambulia mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche na wa Arumeru Mashariki, Joshua Nasari.
Alimshangaa Heche kwa kuomba muongozo kutokana na wananchi wa jimbo lake kuvamia mgodi wa North Mara ulio chini ya kampuni ya Acacia baada ya kukabiliana na askari polisi.
Mwenyekiti wa kikao hicho, Mussa Azzan Zungu alimtaka kuwasiliana na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba kupata ufafanuzi wa suala hilo kutoka serikalini.
“Huyu Heche aliongea humu ndani kuhusu wananchi wake kulinda mgodi, leo anajikosha kwa kuomba muongozo. Rais hakusema watu wakavamie migodi, hao wakamatwe kama wahalifu wengine. Huyu naye akamatwe na kuunganishwa pamoja na wavamizi hao,” alisema.
Baada ya kauli hiyo, Heche alisimama na kumpa taarifa mbunge huyo kwa kueleza kwamba jina lake linatumika vibaya. Alikumbusha kwamba wananchi wake walifuatilia uwasilishaji wa ripoti ya kamati na kufahamu kwamba kampuni hiyo ni feki.
“Nilisema sisi tumeumizwa, sasa kama unafikiri naogopa kuunganishwa hebu njoo unikamate wewe,” alisema.
Baada ya taarifa hiyo, Jackline alimwambia Heche: “Usinipotezee muda, nina mambo mengi ya kuzungumza.”
Baada ya kuachana na Heche, mbunge huyo alimvaa Nasari kwa kueleza kwamba alitumia dakika 10 alizopewa kulalamika juu ya uharibifu uliofanywa kwenye shamba la maua la mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.
“Hizi ni akili au matope? Wananchi wake hawana changamoto? Ni mambo ya aibu sana,” alisema mbunge huyo akikaribia kuhitimisha mchango wake kwenye mjadala huo.
Kabla hajakaa, sauti ilisikika ikimkumbusha suala la kuliwa kwa fedha za msiba huo, kengele ya kuisha kwa muda wake ikiwa imeshagongwa, alitupa kijembe wa upinzani.
“Nakushukuru sana mwenyekiti, naunga mkono hoja na (wapinzani) waache kula rambirambi za msiba wa Ndesamburo,” alisema Ngonyani.
Kauli hiyo iliwafanya wabunge wa upinzani wacharuke na kumtaka afute maneno hayo.
Alikuwa ni mbunge wa viti maalumu (Chadema), Cecilia Pareso aliyemng’ang’ania baada ya kutoa taarifa kwamba kilichozungumzwa na Jackline si sahihi na kumtaka kufuta maneno hayo au kuthibitisha tuhuma hizo.
Mbunge huyo alikubali kuyaondoa maneno yake kwenye kumbukumbu kutokana na kukosa ushahidi wa alichokisema.
“Mwenyekiti, kwa sababu ni suala la msiba, nayaondoa maneno hayo,” alisema na kuhitimisha suala hilo lililowagusa wabunge wengi wa upinzani waliokuwapo kwenye kikao cha jana asubuhi.
No comments:
Post a Comment