Kampuni ya Acacia imeeleza kuwa imepokea taarifa kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inayoonyesha kuwa migodi yake ya Bulyanhulu inadaiwa kodi ya kati ya mwaka 2000 hadi 2017 na Pangea inadaiwa kodi ya kati ya 2007-2017.
Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa katika tovuti ya Acacia jana Julai 24, imeeleza kuwa taarifa hiyo imetokana na ripoti za kamati mbili za Rais zilizoonyesha kuwa wamekuwa hawatangazi kiasi halisi cha mapato yao wakisafirisha mchanga kwenda nje ya nchi.
Acacia wamesema kuwa, bado wanaendelea na msimamo wao wa kupinga matokeo ya kamati hizo na kusema kuwa wamekuwa wakitangaza mapato yao.
Aidha, wameeleza kwamba bado hawajapata nakala za ripoti za kamati ya kwanza na ya pili zilizowasilishwa kwa Rais Magufuli Mei 24 na Juni 12 mwaka huu.
Uchambuzi uliofanywa na TRA umeonyesha kuwa Mgodi wa Bulyanhulu unadaiwa na serikali takribani Tsh 344.8 trilioni (USD 154bn) na Mgodi wa Pangea takribani Tsh 76.1 trilioni (USD 36bn).
Uchambuzi huo unaonyesha kuwa Acacia wanadaiwa takribani Tsh 89.5 trilioni (USD 40bn), ikiwa ni malimbikizo ya kodi na Tsh 335.9 trilioni (USD 150bn) ikiwa ni adhabu na riba.
Aidha, Acacia wamepinga uchambuzi huo, na kusema kuwa wanaufanyia kazi ili waweze kutoa maamuzi sahihi.
No comments:
Post a Comment