Jeshi la polisi nchini Malawi limesema kuwa limepewa kibali maalum cha kumkamata Rais wa zamani wa nchi hiyo, Joyce Banda kwa tuhuma za matumizi mabaya ya ofisi na utakatishaji fedha.
Jeshi hilo limeeleza kuwa limekusanya vielelezo vya kutosha vinavyoonesha kuwa Rais huyo wa zamani ni mhusika katika kashfa kubwa ya rushwa na utakatishaji fedha kiasi cha dola za kimarekani milioni mia mbili na hamsini ($250m), katika kashfa inayofahamika kwa jina la ‘cashgate scandal’.
“Jeshi la polisi la Malawi linapenda kuwafahamisha wananchi kuwa kitengo chake cha kupambana na rushwa na udanganyifu kimefanya uchunguzi kuhusu tuhuma dhidi ya Rais Mstaafu, Joyce Banda na kimepata vielelezo vya kuaminika,” imeeleza sehemu ya taarifa ya polisi kwa umma.
“Vielelezo vilivyokusanywa vinaweza kuonesha kuwa Rais Mstaafu alifanya makosa yanayohusu matumizi mabaya ya ofisi na utakatishaji fedha,” aliongeza.
Mama Banda yuko nje ya nchi hiyo lakini polisi wamesema kuwa watatumia mfumo wa polisi wa kimataifa (Interpol) kusaidia kumrejesha nyumbani ili ajibu tuhuma hizo dhidi yake.
‘cashgate scandal’ ni kashfa kubwa ya rushwa kuwahi kutokea katika historia ya Malawi inayohusisha vigogo wa serikali.
No comments:
Post a Comment