Makamu wa pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi amesema ipo haja kwa Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuangalia uwezekano wa kuondoa kodi ya ongezeko la thamani (Vat) kwa wawekezaji wa makazi nchini ili kuharakisha upatikanaji wa makazi bora kwa wananchi.
Balozi Iddi alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam wakati akizindua mradi wa nyumba za makazi unaofahamika kama Hamidu City Park uliopo wilayani Kigamboni. Mradi huo unatekelezwa na Kampuni ya Orange Tanzania Limited unalenga kujenga nyumba za kisasa zaidi 1,560.
“Makazi bora ni haki ya kila Mtanzania hivyo sisi kama Serikali ni wajibu wetu kila siku kufikiria sera bora zitakazo wawezesha wananchi kufanikisha hilo,’’ alisema.
Alisema kuna haja ya Taifa kuwekeza zaidi kwenye mipango miji inayowaunganisha Watanzania, badala ya ile inayowatenganisha kulingana na vipato.
“Sifa ya miji mizuri ni pamoja mwingiliano wa makazi kati ya watu wenye vipato tofauti, hatuhitaji kuwa na miji inayowatenganisha watu,’’ alisisitiza.
Akizindua nyumba 20 za awali, Balozi Iddi aliipongeza kampuni hiyo kupitia Mkurugenzi wake mkuu, Hamidu Mvungi kwa uzalendo wake wa kuwekeza katika taifa lake huku akiahidi kumuunga mkono kwa kununua nyumba moja.
Akizungumzia mradi huo uliopo kilomita 16 tu kutoka eneo la Feri na kilomita 12 kutoka Daraja la Nyerere, Hamidu alisema unahusisha eneo la zaidi ya eka 130 na utatekelezwa kwa awamu tano tofauti.
“ Awamu ya kwanza itahusisha ujenzi wa nyumba zaidi ya 150 ambazo zitauzwa kati ya mil 120 hadi mil 370 ,’’ alitaja huku akisifia ubora, usalama na baadhi ya huduma za kisasa ikiwemo viwanja vya michezo vitakavyohusishwa katika mradi huo.
Hata hivyo, aliiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kupunguza kama siyo kuondoa kabisa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) ambayo imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la bei kwenye nyumba za makazi.
Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Hashim Mgandilwa.
No comments:
Post a Comment