Wakati mbunge wa Singida Kaskazini (CCM), Lazaro Nyalandu akieleza kuwa anakusudia kuwasilisha hoja ya muswada binafsi kwa Spika utakaoweka sharti la kurejea upya mjadala wa Katiba mpya, utafiti umeonyesha kuwa wananchi wawili kati ya watatu wanasema Tanzania inahitaji Katiba mpya.
Pia, nusu ya wananchi wanasema mchakato wa Katiba uanze upya na tume mpya.
Jana kupitia katika akaunti zake za mitandao ya kijamii ya Instagram, Twitter na Facebook Nyalandu aliandika, “Nakusudia kuwasilisha kwa Spika wa Bunge, mheshimiwa Job Ndugai azma yangu ya kuleta muswada binafsi wa sheria katika kikao kijacho cha Bunge itakayoweka sharti la kurejea upya mjadala wa Katiba mpya ya Tanzania, kwa kuzingatia rasimu ya Katiba ilivyowasilishwa na Tume ya Jaji Warioba.”
Nyalandu alisema muswada huo anatarajia kuuwasilisha kwenye kikao kijacho cha Bunge.
Akizungumza kwa simu baada ya kuandika maneno hayo, Nyalandu alisema amekusudia kupeleka muswada huo kwa sababu mchakato wa Katiba mpya haukufikia mwisho.
“Nitafurahi sana kama jambo hili litafanikiwa kwa kuwa lina umuhimu wake kwa kila mtu. Suala hili pia halina itikadi za vyama vya siasa na lina masilahi, kwa sababu Katiba ina uwezo wa kukaa zaidi ya miaka 100,” alieleza Nyalandu.
Mbali na Nyalandu kueleza hayo, mwezi uliopita asasi za kiraia zaidi ya 80 zilijitokeza hadharani na kutoa tamko zikisema kwamba huu ni wakati mwafaka wa mchakato wa Katiba kuanza upya ili ifikapo 2020 iwe imepatikana.
Kabla ya asasi hizo kutoa tamko, Jukwaa la Katiba lilijitokeza na kusema litaandaa maandamano ya amani kumueleza Rais John Magufuli umuhimu wa kuandika Katiba mpya.
Mbali na hayo, jana matokeo yaliyotolewa na Twaweza katika utafiti uitwao ‘Zege imelala?’ yameeleza kuwa wananchi wawili kati ya watatu wanasema Tanzania inahitaji Katiba mpya, huku nusu yao wakisema mchakato wa Katiba uanze upya na tume mpya.
Utafiti huo umesema muhtasari unatokana na takwimu kutoka sauti za wananchi ukiwa ni utafiti wa kwanza barani Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaotumia simu za mikononi.
Mkurugenzi mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze alisema, “Wananchi wanataka Katiba mpya. Wengi wao wanataka mchakato uanze upya na tume mpya katika ukurasa mpya. Hata hivyo, wapo wananchi ambao wapo tayari kusonga mbele kwa kutumia rasimu iliyoandaliwa na tume iliyotangulia.”
Pia, alisema kuwa wananchi wanaunga mkono kipengele kilichoongeza madaraka ya Bunge katika suala la kuwapitisha mawaziri walioteuliwa na kinachowapa wananchi haki ya kuwaondoa wabunge wanaozembea kazini.
Eyakuze alisema utafiti umedhihirisha uwajibikaji wa siasa kwenye uhalali wa mchakato wa Katiba.
“Matokeo yameonyesha dhahiri kwamba wananchi wengi wanatatizwa katika kutofautisha kitendo cha Ukawa kugomea Bunge la Katiba na migomo mingineyo. Ushabiki wa kisiasa huwafanya watu wengi kutozingatia uhalali wa jambo husika,” alisema.
Eyakuze alisema, “Hivyo basi; vyovyote tutakavyofufua mchakato wa Katiba ni muhimu kwa wahusika wakuu kuheshimu na kutambua kwamba sheria mama ya nchi ni ya thamani zaidi kuliko tofauti za kisiasa. Tanzania inahitaji mchakato wa Katiba utakaozingatia uhalali na ujumuishi wa Watanzania wote.”
Taarifa ya Twaweza kwa vyombo vya habari ilisema asilimia 67 ya Watanzania wanasema ni muhimu kwa Tanzania kupata Katiba mpya na asilimia 56 wanasema toleo la mwisho la rasimu ya Katiba lipigiwe kura na wananchi.
Hata hivyo, asilimia 48 ya wananchi wanasema kwa maoni yao, Katiba mpya haitapatikana ndani ya miaka mitatu ijayo.
Taarifa hiyo ilisema wananchi wanaendelea kuunga mkono kwa nguvu kubwa uundwaji wa Katiba mpya inayotilia mkazo suala la uwajibikaji.
Ilisema asilimia 79 wanataka mawaziri wanaoteuliwa wapitishwe na Bunge na asilimia 64 wanataka wawe na uwezo wa kuwaondoa wabunge katikati ya mihula yao iwapo hawatatekeleza majukumu yao ipasavyo.
Hata hivyo, wananchi wamegawanyika kwenye baadhi ya hatua za uwajibikaji zilizopendekezwa ikiwamo kuzuia viongozi na watumishi wa umma kuwa na akaunti nje ya nchi (asilimia 52 wanaunga mkono), kuwapo kwa ukomo wa ubunge (asilimia 52 wanaunga mkono) na kuweka kanuni za uwazi na uwajibikaji kuwa sehemu ya tunu za Taifa (asilimia 48 wanaunga mkono).
Hivyo vyote ni vipengele vya rasimu ya Katiba ambavyo viliondolewa na Bunge Maalumu la Katiba.
Twaweza ilisema wananchi pia wanaunga mkono kuondolewa kwa kipengele kinachotaka kuchunguza na kudhibiti ofisi ya Rais (asilimia 55) na mawaziri kuchaguliwa kutoka nje ya Bunge (asilimia 62).
Matokeo hayo taasisi hiyo imesema yanatokana na takwimu zilizokusanywa kutoka kwa wahojiwa 1,745 kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara (Zanzibar haihusiki kwenye utafiti huu) Juni hadi Julai 2017.
Kuhusu muundo wa Serikali ni moja kati ya vipengele vilivyoibua mjadala mzito wakati wa mchakato wa kuunda Katiba mpya na hatimaye kuwagawa wananchi. Asilimia 42 ya wananchi wa Tanzania Bara waliunga mkono muundo wa Serikali mbili.
Twaweza imesema muundo wa Serikali moja ulikubalika kwa asilimia 25 na ule wa Serikali tatu uliopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ulipendwa na asilimia 16.
Mchakato wa Katiba mpya ulisimama Oktoba 2014 baada ya Tume ya Uchaguzi kudai kuwa ungeiliana na Uchaguzi Mkuu wa 2015.
No comments:
Post a Comment