Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Udaktari cha Imtu, Daniel Mabisi (28) anadaiwa kujinyonga kutokana na kufeli mitihani.
Mabisi ambaye ni mkazi wa mtaa wa Mgeninani, Kata ya Kijichi jijini Dar es salaam anadaiwa kukutwa amejinyonga jana saa saba mchana maeneo ya Mgeninani.
Taarifa zilizopatikana zinadai siku mbili kabla ya kujinyonga, mwanafunzi huyo alionekana mtaani hapo baada ya kutoka chuo alikokuwa akisoma.
Inaelezwa kuwa mwanafunzi huyo amefeli mara mbili mfululizo.
Akizungumza kwa simu kutoka Morogoro, baba mdogo wa marehemu, Joseph Lukuba alisema amepokea kwa mshtuko taarifa za mtoto wake.
“Nimepigiwa simu mchana huu nikaambiwa Daniel amejinyonga, nimeshtuka kwa sababu ni juzi tu tulimtumia nauli ili arudi nyumbani Mwanza baada ya kupata taarifa kuwa amefeli kwa mara nyingine,” alisema Lukuba.
Alisema uamuzi aliouchukua unasikitisha kwa kuwa kufeli, isingekuwa sababu ya kushindwa maisha hadi kufikia uamuzi wa kujinyonga.
“Kama familia tumehama na tuko mbali kikazi, tumemuomba jirani asimamie suala hili wakati taratibu za mazishi au kusafirisha mwili zikiendelea,” alisema.
Akizungumzia tukio hilo, mwenyekiti wa Mtaa wa Mgeninani, Khuruka Mwinyimvua alisema baada ya kupata taarifa hizo alifika eneo la tukio na kukuta mwili ukiwa umening’inia juu ya mwembe.
“Kijana huyo alionekana tangu juzi akizunguka mtaani hapa baada kurejea kutoka chuoni anakosoma, alionekana kama mtu asiyekuwa na furaha,” alisema Mwinyimvua na kuongeza: “Hadi sasa mwili umechukuliwa na polisi kwa taratibu nyingine.”
Naye kamanda wa polisi Mkoa wa Temeke, Emmanuel Lukula alithibitisha kupokea taarifa za kujinyonga kwa kijana huyo na kuwaagiza askari walio karibu na maeneo hayo kuchukua mwili huo.
Na Aurea Simtowe na Asna Kaniki mwananchi
No comments:
Post a Comment