Serikali imefikia uamzi wa kusitisha kuanza kutumika kwa kanuni za leseni ya usafirishaji na kukiri kuwepo kwa mapungufu ya wazi ambayo yanahitaji marekebisho ili kuondoa kasoro zinazoweza kumuonea mmiliki wa chombo husika.
Uamzi huo umefikiwa leo kwenye mkutano wa wamiliki wa vyombo vya usafiri na Naibu waziri wa Uchukuzi na mawasiliano Atashasta Nditiye ambao kwa pamoja wamekubaliana kusitisha kuanza kutumika kwa kanuni hizo ili kuzipitia upya na kuondoa mapungufu.
Moja ya mapungufu ambayo Naibu waziri amekiri kwamba yapo kwenye kanuni hizo ni pamoja na kanuni ambayo inaeleza mmiliki wa gari kutozwa faini ya hadi ya shilingi laki mbili na nusu kwa makosa ya dereva.
Aidha Nditiye amedai kuwa ni kweli kanuni hizo zilizotolewa na mamlaka ya udhibiti wa usafiri wa nchi kavu na majini SUMATRA, zingeleta changamoto katika uendeshaji wa vyombo vya moto. Waziri Nditiye ameagiza kufanyika marekebisho ya kanuni hizo hadi kufikia Desemba 1 mwaka 2017.
Kanuni hizo zilipaswa kuanza kutumika hivi karibuni hali ambayo ilipelekea wamiliki wa vyombo vya usafiri kutangaza azima ya kuitisha mgomo kwa madai ya kutosikilizwa kila mara wanapotoa maoni yao juu ya kanuni hizo za usafirishaji.
No comments:
Post a Comment