Wakati uongozi wa kata ya Nyehunge wilayani Sengerema ukipitisha sheria ya kuwacharaza viboko 12 au faini ya Sh10,000 wanaume watakaokutwa wamesimama na wanafunzi wa kike, Wilaya ya Tandahimba imekamata wanafunzi watano waliopata ujauzito mwaka jana.
Sheria hiyo ndogo imepitishwa juzi kwenye kikao cha maendeleo ya kata (WODC) baada ya tatizo la wanafunzi kukatisha masomo kutokana na kupata uja uzito kuzidi kuwa sugu.
Ofisa mtendaji wa Kata ya Nyehunge, Mabula Enock alisema sheria hiyo itasaidia kudhibiti vitendo vya wanaume wanaoshawishi wasichana kufanya nao mapenzi na baadaye kuwapa ujauzito unaokatisha ndoto zao.
“Tumelazimika kupitisha sheria hiyo ili kuungana na mkuu wa wilaya yetu, Emmanuel Kipole aliyeagiza wanaume watakaokutwa wamesimama na wanafunzi wacharazwe viboko au kutozwa faini ya Sh10, 000 ama vyote kwa pamoja,” alisema Enock
Agizo la mkuu huyo wa wilaya alilitoa Oktoba mwaka 2017 wakati akikaribisha wanafunzi 81 kujiunga na masomo ya kidato cha tano katika Shule ya Sekondari ya Nyehunge.
Mkazi wa kata hiyo, Mussa Kazimili alisema sheria hiyo ndogo itasaidia kupunguza tatizo hilo na kuwataka wananchi na wazazi kusaidia kubaini wanaume watakogundulika kufanya vitendo hivyo.
Diwani wa kata hiyo, Charles Mbogo alisema kitendo cha kukatiza masomo si cha kuungwa mkono, hivyo adhabu inapaswa kuongezwa na kuitaka jamii kuachana na suala hilo.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na ofisa elimu ya sekondari wa Buchosa, Benjamini Siperato halmashauri hiyo ina jumla ya wanafunzi 1,136 katika shule 20 za sekondari 20 na mwaka 2016/17 wanafunzi 18 wa kike walipata ujauzito, hivyo jamii inapaswa kuacha tabia ya kuwarubuni watoto wa kike.
Wakati huohuo, serikali wilayani Tandahimba imewakamata wanafunzi watano waliopata ujauzito kwa lengo la kutaka habari kuhusu wanaume waliowapa ujauzito na kukatiza masomo yao.
Katibu tawala wa wilaya hiyo, Mohamed Azizi, ambaye alikuwa akizungumza kwa niaba ya mkuu wa wilaya ya Tandahimba, Sebastian Waryuba, alisema wanafunzi ha walikamatwa na watoto wao, lakini wahusika hawajakamatwa.
“Tumefanikiwa kuwakamata wazazi na wanafunzi watano wakiwa wamejifungua. Kati yao, mmoja aliacha shule akiwa kidato cha nne,” alisema.
“Wengine watatu wa kidato cha pili. Baada ya kuzungumza nao wamesema hawapati huduma zozote kutoka kwa wahusika ambao wamewapa ujauzito. Hali hiyo ni wazi kuwa inawapa shida wazazi.”
Alisema wazazi wamekuwa wakilaumiwa kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo ili kuhakikisha watoto wao wanamaliza elimu ya sekondari bila kupata ujauzito.
“Inasikitisha. Mmoja ameacha shule akiwa kidato cha nne mwaka jana, alibakiza siku chache tu aweze kumaliza masomo yake. Hili liwe somo kwa wazazi na wanafunzi wengine.
Na Daniel Makaka na Mary Sanyiwa, Mwananchi
No comments:
Post a Comment