Asa Mwaipopo
Kampuni ya madini ya Acacia imemtangaza aliyekuwa meneja mkuu wa uendelevu, Asa Mwaipopo kuwa mkurugenzi mtendaji wake Tanzania.
Taarifa ya uteuzi huo imeambatana na ripoti ya matokeo ya hesabu za fedha kwa miezi 12 ilioishia Desemba 2017 iliyotolewa na ofisa mtendaji mkuu, Peter Geleta.
Katika ripoti hiyo iliyotolewa jana, Geleta alisema anaamini zuio la kusafirisha mchanga wa dhahabu (makinikia) huenda likaondolewa mwaka huu kutokana na mazungumzo yanayoendelea baina ya Barrick na Serikali ya Tanzania.
Uteuzi wa Mwaipopo ni mkakati wa kampuni hiyo wa kuhakikisha miradi yote nchini inaendeshwa na wafanyakazi wa ndani badala ya wageni ulioanza kutekelezwa miaka minne iliyopita.
Hadi sasa kampuni hiyo imeripoti kuwa idadi ya wafanyakazi wa kigeni imepungua kutoka asilimia 15 miaka minne iliyopita hadi nne mwaka jana.
Kwa mujibu wa hesabu za kampuni hiyo za mwaka 2017, biashara iligubikwa na changamoto nyingi zilizosababisha ishindwe kutoa gawio kwa wanahisa wake.
“Mwaka ulioisha, akiba ya fedha katika kampuni ilishuka kutoka Sh700 bilioni hadi Sh180 bilioni, upungufu wa Sh520 bilioni kwa mwaka ukijumuisha ongezeko la kodi ya thamani. Kutokana na haya, bodi ya wakurugenzi imeamua kutotoa gawio la faida la mwisho wa mwaka kwa wanahisa,” alisema Geleta.
“Tunaendelea kutathmini hatua za kulinda mzunguko wa fedha pamoja na kupunguza gharama za uendeshaji wa kampuni, uchimbaji wa upanuzi huko North Mara, utafiti wa machimbo mapya na kulinda thamani ya dhahabu dhidi ya kushuka kwa bei kwenye masoko ya kimataifa.”
Alisema kwa kuzingatia viwango vinavyotumika vya kihasibu, wamerudia hesabu ya thamani ya mali zao kwa kulinganisha na vipengele vichache vya mpango uliyotangazwa na Barrick na Serikali ya Tanzania wakati wa makubaliano yao, matokeo yameonyesha kupungua kwa thamani ya mali zao zote.
“Athari kubwa ipo katika mgodi wetu wa Bulyanhulu, kutokana na hatua ya kupunguza uzalishaji na uhai wa mgodi wenyewe. Upungufu huu umepelekea thamani ya sasa ya mgodi kutoka Dola za Kimarekani 1.2 bilioni hadi Dola za Kimarekani 600 milioni, Pia tumeona nyongeza ya matumizi ya Dola za kimarekani 12 milioni (Sh25 milioni) kwa mradi wa Nyanzaga ikiakisi athari za sheria mpya za madini za thamani ya sasa ya mradi, Mporomoko huu wa thamani ya mali zetu hauna athari katika mapato yetu,” alisema Geleta.
Hata hivyo, Acacia ilisema bado inasubiri matokeo ya mazungumzo na mapendekezo yaliyofikwa kati ya Barrick na Serikali ya Tanzania kwa ajili ya mapitio kabla ya kutekelezwa.
Alisema kampuni hiyo imeendelea kuwa na nidhamu kwenye matumizi na kuchukua hatua kadhaa kuhakikisha biashara yao inaendelea kukua.
Matarajio ni kwamba Barrick inategemea kuwasilisha mapendekezo ya mazungumzo yake na serikali ya Tanzania kwenye kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2018.
“Tunaendelea kutathmini hatua zaidi za kulinda mzunguko wa fedha pamoja na kupunguza gharama za uendeshaji wa kampuni, uchimbaji wa upanuzi huko North Mara, utafiti wa machimbo mapya pamoja na kulinda thamani ya dhahabu dhidi ya kushuka kwa bei kwenye masoko ya kimataifa,” alisema Geleta.
Na Ephrahim Bahemu, Mwananchi
No comments:
Post a Comment