Kesi ya msanii Wema Sepetu ya kukutwa na msokoto wa bangi imesikilizwa jana February 8, 2018 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambapo Inspekta wa Polisi, Wille aliieleza Mahakama kuwa hakuwepo wakati Wema akichukuliwa sampuli ya mkojo kwa Mkemia Mkuu wa serikali.
Shahidi huyo aliyaeleza hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba wakati alipoulizwa maswali na Wakili wa Wema, Alberto Msando.
Katika ushahidi wake, Inspekta Wille, alidai hakuwahi kupeleka sampuli za mkojo za washtakiwa wenzake Wema ambao ni Angelina Msigwa na Matrida Abbas kwenda kuchunguzwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali.
Shahidi huyo alidai kuwa aliijaza fomu ya kupeleka sampuli ya mkojo wa Wema saa nne asubuhi akiwa ofisini kwake na kuandika maneno mkojo uko ndani ya chupa ya plastiki.
==>Mahojiano kati ya wakili Msando na shahidi yalikuwa hivi:
Wakili: Katika hii fomu shahidi umejaza kuwa mkojo ulikuwa ndani ya chupa ya plastiki. Nataka kujua je uliuona huo mkojo kama ni wa Wema?
Shahidi: Nilijaza fomu kutokana na uzoefu wangu wa miaka 15.
Wakili: Ulijaza fomu ya kisheria ya kupima sampuli kabla ya mshtakiwa kufika kwa Mkemia Mkuu wa Serikali?
Shahidi: Ndio uzoefu wangu.
Wakili: Mkojo uliokabidhi uliupata wapi?
Shahidi:Kwa Mkemia Mkuu wa Serikali.
Wakili: Je ulikuwapo wakati mshtakiwa anachukuliwa sampuli ya mkojo?
Shahidi : Sikuwapo.
Wakili: Inawezekana ukasema hujui kilichokuwa ndani ya chupa ya plastiki kwa vile haukuwapo?
Shahidi: Sijui.
Wakili: Wakati Mkemia Mkuu unamkabidhi mkojo chupa ya plastiki ilikuwa imewekwa lakiri?
Shahidi: Ndiyo
Wakili: Je, ulikaa muda gani katika ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali?
Shahidi: Niliondoka baada ya kukabidhi fomu, ilikuwa kama saa 5:00 asubuhi.
Wakili: Ulihusika kwenda kukagua nyumbani kwa mshtakiwa wa kwanza?
Shahidi: Ndiyo.
Wakili: Je, ulipekua chumba anacholala mshtakiwa wa kwanza?
Shahidi: Hapana.
Wakili: Je, vitu mlivyokuta katika upekuzi wenu vilikutwa sehemu gani?
Shahidi: Katika upekuzi msokoto wa bangi na rizza ya kusokotea bangi ilikutwa jikoni juu ya kabati la vyombo na walikuta msokoto wa bangi uliotumika ukiwa ndani ya kiberiti dirishani katika chumba wanacholala wafanyakazi wake.
Wakili: Je, kwenye hicho chumba mlichokuta msokoto ni wa mshtakiwa wa pili au wa tatu?
Shahidi: Sijui.
Wakili: Je, huo msokoto ni wa mshtakiwa wa kwanza?
Shahidi: Sijui.
Wakili: Je mshtakiwa wa pili na watatu alipimwa sampuli ya mkojo?
Shahidi: Hapana.
Mahakama iliipokea hati ya ukamataji mali iliyojazwa katika upekuzi uliofanyika nyumbani kwa Wema Sepetu kama kielelezo.
Kesi imeahirishwa hadi Februari 26 na 27, mwaka huu itakapoendelea kusikilizwa kwa ushahidi wa upande wa mashtaka.
No comments:
Post a Comment