WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
ameitaka Halmashauri ya wilaya ya Temeke kuondoa wafanyakazi wa mkataba kwa ili kuwapa
ajira ya kudumu kwa wenye sifa na kuwaondoa wasiokuwa na sifa ifikapo Julai 30
mwaka huu.
Amesema kitendo cha kutowaajiri na
kuwatumikisha kwa mikataba kwa muda mrefu kinasababisha wakose stahiki zao
jambo ambalo halikubaliki.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana(Alhamisi,
Julai 28, 2016) wakati akizungumza na watumishi wa halmashauri hiyo na
kusisitiza kwamba ni lazima sula hilo lishughulikiwe haraka kwa sababu hayo
ndio matundu watumishi hewa.
“Mnawatumikisha
watu kama vibarua kwa muda mrefu, hapa kuna wengine wanafanya kazi kwa mikataba
kwa miaka mitano hadi sita hii haikubaliki kwani mnawakosesha stahili zao pale
mnapowaachisha kazi,” alisema.
Awali Kaimu Ofisa Utumishi wa
Manispaa hiyo Zaitun Hassan alisema wamekuwa wakitoa ajira za mikataba kwa
sababu wamekosa watu wenye sifa za kuweza kuajiriwa hususan madereva.
“Kwa mara ya
mwisho umetangaza lini nafasi za ajira? Katika mkoa wa Dar es Salaam kweli
wanaweza kukosekana madereva wenye sifa za kuajiriwa? Alihoji
Waziri Mkuu.
Zaitun alisema kuwa madereva wengi
wanaojitokeza pindi wanapotangaza ajira wanashindwa kufikia vigezo ikiwemo kuwa
na cheti cha VETA na badala yake wanakuwa na cheti cha kidato cha nne tu.
Hata hivyo, Waziri Mkuu alisema
kuwa kuna wafanyakazi wengine katika Idara ya Uhasibu na Ujenzi ambao nao
wameajiriwa kwa mkataba hivyo amemtaka Ofisa Utumishi kuomba kibali cha kuajiri
kwa Katibu Mkuu Utumishi.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu
amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kufanya tathmini ya
maeneo yote ya shule kwenye mkoa wake na watakaobainika kuingia katika maeneo
hayo waondolewe haraka.
Alisema baada ya kukamilisha
utengenezaji wa madawati kinachofuatia sasa ni ujenzi wa vyumba vya madarasa,
ambapo amezitaka halmashauri kuweka mipango ya kujenga majengo ya madarasa ya
ghorofa ili waweze kuwa na madarasa mengi katika eneo dogo.
Awali Waziri Mkuu alipokea msaada
wa madawati 705 katika hafla iliyofanyika kwenye viwanja vya shule ya msingi
Chamazi wilayani Temeke ambapo kati yake Ubalozi wa Kuwait nchini Tanzania
umetoa madawati 600 na Jumuia ya Mabohora imetoa madawati 105.
Pia Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dk. Agustino Mahiga alimkabidhi Waziri
Mkuu hundi ya sh. milioni 85 fedha zilizochangwa na watumishi wa wizara hiyo
kwa ajili ya kuchangia utengenezaji wa madawati.
Dk. Mahija alisema watumishi hao
walichanga sh. milioni 100 kwa ajili ya utengenezaji wa madawati ambapo sh.
milioni 15 wamekabidhi kwa mkuu wa wilaya ya Manyoni Geofrey Mwambe ambaye
alikuwa mtumishi wa wizara hiyo ili naye akatengeneze madawati kwa shule za
wilayani kwake.
Kwa upande wake Balozi wa Kuwait
nchini Jaseem Al Najem amesema Serikali ya Kuwait itaendelea kushirikiana na
Serikali ya Tanzania katika shughuli zote za maendeleo hususan katika sekta za
elimu na afya.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
No comments:
Post a Comment