
WATU watatu wamekufa baada ya
kufukiwa na mizigo wakati lori walilokuwa wamepanda kutoka Mnada wa Mgaga
wilayani Bahi mkoani Dodoma, kupasuka tairi na kupinduka.
Ajali hiyo iliyotokea katika Kijiji
cha Chifutuka saa 11 jioni juzi, pia ilisababisha majeruhi 19 ambao
wamekimbizwa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kwa matibabu.
Akithibitisha kutokea kwa ajali
hiyo, Mrakibu Mwandamizi wa Jeshi la Polisi mkoani hapa, Mayala Towo alilitaja
lori lililohusika kuwa ni aina ya Mitsubishi Fuso lenye namba za usajili T 689
BEG.
Alisema lori hilo lilipofika eneo
la Chifutuka wilayani Bahi, tairi lake la mbele lilichomoka na kupinduka.
“Gari hilo lilichomoka tairi ya
mbele na kusababisha kupinduka kisha mizigo kuwaangukiwa watu waliokuwepo
katika lori hilo ambapo watu watatu wamekufa na majeruhi 19 walipelekwa katika
Hospitali ya Mkoa,”alisema Towo.
Akizungumza na waandishi wa habari
jana katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Mganga Mfawidhi wa Hospitali
hiyo, Dk Zainabu Chaula alisema juzi saa mbili usiku walipokea majeruhi 19 na
maiti watatu.
Dk Chaula alitaja waliokufa kuwa ni
Isdori Thomas Motto (38), Michael Msongela (29) na Elias Masimo Petro (51) wote
wakazi wa Dodoma.
Daktari huyo alisema majeruhi 12
walitibiwa na kuruhusiwa huku wengine wakilazwa wodi namba 10, 8 na 11 kwa
ajili ya uangalizi zaidi.
Aliwataja waliolazwa kuwa ni Muoni
Magege (40) mkazi wa Dar es Salaam, Suzy, Samweli (16), Frida Chipaga, Chausiku
Mohammed (38), Josephine Sakiru (43), Selemani Salum (35) na Elias Petro (51)
wote wakazi wa Dodoma.
Akisimulia ajali hiyo, mmoja wa
majeruhi ambaye amelazwa katika Wodi Namba 8, Chausiku Mohammed mkazi wa
Chinangali mjini Dodoma, alisema walipanda lori hilo lililokuwa likitoka
mnadani na kwamba alichokiona ni kuchomoka kwa tairi la lori hilo, hivyo gari
kupinduka na wao kufunikwa na mizigo iliyokuwepo katika lori hilo.
“Mimi nilienda mnadani kwa ajili ya
kununua mazao, kama unavyojua malori ya minadani yanabeba kila kitu hadi mizigo
sasa sisi kilichotuumiza ni mizigo kwani ilitulalia na mimi kama unavyoona
nimeumia huu upande wote wa kulia na hapa katika mkono wangu,”alisema Chausiku.
Seleman Salum aliyelazwa Wodi Namba
11 mkazi wa Uwanja wa Ndege, alisema ajali hiyo ilisababishwa na kuchomoka kwa
tairi la mbele na kupinduka. Alisema ajali hiyo ilitokea majira ya saa 11 jioni
karibu na Kijiji cha Chifutuka wilayani Bahi.

No comments:
Post a Comment