WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa
amepiga marufuku matumizi ya viberiti, mishumaa na hita za kuchemshia maji kwa
wanafunzi wa bweni ili kuepusha majanga ya moto na atakayekutwa, atachukuliwa
hatua kali.
“Kuna tabia ya baadhi ya wanafunzi
hasa wa masomo ya fizikia kutengeneza vifaa vya kienyeji vya kuchemsha maji
mabwenini, jambo hili ni la hatari kwani linaweza kusababisha ajali ya moto,
hivyo ni marukufu kwa mwanafunzi kutumia vifaa hivyo,” alisema.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana
katika harambee ya kuchangisha fedha za ujenzi wa majengo ya Shule ya Sekondari
Lindi, yaliyoungua moto usiku wa kuamkia Julai 10, mwaka huu.
Katika ajali hiyo shule imeathirika
kwa asilimia 34 baada ya vyumba tisa vya madarasa, jengo lenye matundu 26 ya
vyoo na jengo la maabara ya kemia na fizikia yameungua na kusababishia hasara
ya Sh milioni 682.78.
Waziri Mkuu alisema kwa namna
ambavyo majengo hayo yameungua, ni vema yakavunjwa na kujengwa upya. Aliwataka
kutumia nafasi hiyo kujenga jengo la ghorofa ili kutumia eneo dogo kwa kujenga
madarasa mengi.
Pia alimuagiza Mkuu wa Mkoa wa
Lindi, Godfrey Zambi kuhakikisha fedha zitakazopatikana katika harambee hiyo,
zinatumika kama ilivyokusudiwa.
Harambee ilihudhuriwa na mke wa
Waziri Mkuu, Mary Majaliwa, mke wa Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Mama Salma
Kikwete, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Halima Dendego na wadau wa maendeleo na
wanafunzi waliosoma shule hiyo akiwemo Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,
Ramo Makani.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu
amezitaka taasisi mbalimbali nchini kufunga vifaa vya kuzimia moto katika
majengo yao kwa ajili ya kuvitumia pindi ajali za moto zinapotokea.

No comments:
Post a Comment