
Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima ambaye amekuwa akitafutwa na Jeshi la Polisi kwa siku kadhaa alikamatwa jana katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA) alipowasili akitokea Japan.
Baada ya Askofu Gwajima kukamatwa
na Kikosi cha Polisi cha Uwanja wa JNIA alipelekwa moja kwa moja Kituo Kikuu
cha Polisi kwa ajili ya mahojiano akidaiwa alitoa maneno ya uchochezi mwezi
uliopita.
Akizungumzia kukamatwa kwake,
Kamanda wa Polisi Uwanja wa JNIA, Martin Otieno alisema askofu huyo aliwasili
saa 2.45 asubuhi akitokea Japan kwa kutumia ndege ya Shirika la Ndege la Kenya.
Otieno alisema mara baada ya
kukamatwa alipelekwa katika Kituo Kikuu cha Polisi kwa ajili ya kuhojiwa na
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.
“Ni kweli tulimkamata Askofu
Gwajima hapa uwanja wa ndege wa JNIA baada ya kuwasili kwa ndege ya Shirika la
Ndege la Kenya na tulipomuhoji alidai kuwa alikuwa nchini Japan,” alisema Otieno.
Mwanasheria wake Peter Kibatala
alisema Gwajima alifika Kituo Kikuu cha Polisi saa 4.45 asubuhi kwa mahojiano
mafupi na aliruhusiwa kuondoka baada ya kujidhamini yeye mwenyewe.
“Askofu Gwajima amehojiwa leo
(jana) na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu na amejidhamini yeye mwenyewe,
ameruhusiwa kuondoka hivyo tunasubiri chochote kitakachoendelea,” alisema
Kibatala bila kueleza mahojiano yalivyokuwa.
Askofu Gwajima alikuwa anatafutwa
na polisi tangu mwezi uliopita baada ya kusambazwa mkanda kwenye mitandao ya
kijamii unaodhaniwa una sauti yake akipendekeza Rais mstaafu Jakaya Kikwete
kufikishwa mahakamani kwa yote yaliyofanyika wakati wa utawala wake ambayo sasa
Rais John Magufuli anayashughulikia kwa mtindo wa kutumbua majipu.
Katika mkanda huo, sauti hiyo
inadai kuwa baadhi ya viongozi wa CCM wametuma watu mikoani kupiga kampeni ya
kutaka Rais Magufuli asipewe uongozi wa chama hicho kwa sasa kama ilivyo
utaratibu wa chama hicho na kwamba hilo likifanyika basi Rais abadili katiba
ili mstaafu huyo aweze kufikishwa kortini.
Tangu ulipotolewa mkanda huo,
makachero wa polisi wamekuwa wakipiga kambi nyumbani kwa Askofu Gwajima kwa
lengo la kumkamata lakini hawakumpata.
Baadaye ilikuja kufahamika kwamba
askofu huyo alikuwa amekwenda nje ya nchi lakini haikujulikana ni nchi gani.
Hata hivyo, baada ya kutafutwa na
polisi, Gwajima kupitia wakili wake Kibatala alisema atakaporejea nchini
atakwenda moja kwa moja polisi kwa ajili ya mahojiano.
Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es
Salaam, Simon Sirro amekuwa akisisitiza kwamba jeshi litaendelea kumtafuta
askofu huyo kwa kushirikiana na polisi wa kimataifa, Interpol.

No comments:
Post a Comment