WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dk
Harrison Mwakyembe amesema jumla ya watuhumiwa 30 wa mauaji ya vikongwe na
wenye ulemavu wa ngozi (albino) nchini, wamehukumiwa kunyongwa, baada ya
kupatikana na hatia ya mauaji hayo.
Dk Mwakyembe amesema pia kuwa
serikali itaendelea kutoa adhabu kali kwa watu watakaobainika kuendelea
kuhusika na mauaji ya watu hao ili kumaliza tatizo hilo, ambalo limeipaka
matope Tanzania kwa kuonekana sio kisiwa tena cha amani. Waziri huyo alisema
hayo mjini Shinyanga jana, alipofanya ziara yake ya kikazi.
Alisema katika miaka ya hivi
karibuni tatizo la mauaji ya wenye ualbino na vikongwe yamepungua nchini na
kwamba watahakikisha wanayakomesha kwa kutoa adhabu kali kwa wauaji.
“Tatizo hili la mauaji ya vikongwe
na albino linatutia sana doa nchi yetu kimataifa ambayo imekuwa ikisifika kwa
amani na utulivu, hivyo natoa mwito kwa wananchi waachane na mauaji ya watu
hawa wasio na hatia pamoja na mahakama zifanye kazi kwa kutoa hukumu za haraka
kwa watu watakaohusika na mauaji hayo,” alisema Dk Mwakyembe.
Hata hivyo, Dk Mwakyembe alisema
serikali itaanza mikakati ya kujenga mahakama za mwanzo kwa kila kata nchi
nzima ili kuondoa misongamano za kesi mahakamani na kukarabati majengo ya
mahakama ambayo yamechakaa.
Aliwataka wakuu wa wilaya, waunde
kamati za maadili ya wilaya.
Akisoma taarifa ya mkoa, Mkuu wa
Mkoa wa Shinyanga, Zainabu Telack, alitaja changamoto ambazo zinawakabili kuwa
ni uchakavu wa majengo ya mahakama, uhaba wa mahakimu na magereza ya Shinyanga
na Kahama kuwa finyu na hivyo kusababisha mlundikano wa wafungwa.

No comments:
Post a Comment