
Askofu wa Kanisa la Ufufuo na
Uzima, Josephat Gwajima amemjibu katibu mkuu wa zamani wa CCM, Yusuf Makamba
aliyemtuhumu kuwa ni mwongo akisema leseni yake ni ya kuendesha magari makubwa
na siyo vibajaji na maguta.
Akihubiri katika kanisa lake jana,
Gwajima bila kutaja jina la Makamba, alisema: “Siwezi kushughulika na
vigari vidogovidogo nyie mnanifahamu, mimi nina leseni ya kuendesha semi
trailer …nadhani mmenielewa,” alisema huku waumini wake
wakimshangilia.
Juzi, Makamba aliwaeleza wajumbe wa
Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM kuwa Askofu Gwajima ni kiongozi wa dini lakini ni
muongo na kuwa uongo wake unawaudhi hata waumini wake ambao ni wanachama wa
chama hicho.
Alisema Gwajima amekuwa akisema
uongo kuwa Rais mstaafu, Jakaya Kikwete hataki kuachia madaraka ya uenyekiti wa
chama hicho, kitu ambacho Rais huyo mstaafu alikanusha akisema ni yeye
alikwenda kumshawishi Dk John Magufuli kuchukua nafasi hiyo kabla ya muda wa
uliopangwa kikatiba.
Katika mahubiri hayo, Gwajima pia
alisema mafunzo aliyoyapata tangu akiwa mdogo ni kuogopa kugombana na watu wa
aina tatu, walevi, wazee na wagonjwa.
“Baba yangu alinifundisha
nisigombane na walevi, wazee na wagonjwa kwani ukimpiga kidogo mtu wa aina hiyo
anaweza kufa,” alisema Gwajima.
“Hata nyie waumini wangu nawaomba
msigombane na watu wa aina hiyo kwani mnaweza kupata matatizo,” alisema.
Kiongozi huyo aliongoza mamia ya
waumini wake kumuombea Rais Magufuli kwa kushinda uenyekiti wa CCM akisema kofia
hizo mbili zimempa meno ya kung’ata na zitamwongezea kasi ya kutatua matatizo
ya wanyonge nchini.
Rais Magufuli juzi alichaguliwa
kuwa Mwenyekiti wa CCM baada ya kupata kura zote 2,398 alizopigiwa na wajumbe
wa mkutano huo.
Kutokana na ushindi huo, Gwajima
alisema Magufuli amepewa meno ya `kung’ata’ kila upande tofauti na alipokuwa na
kofia moja ya urais.
Alisema kwa muda mfupi aliokaa
madarakani, elimu ya msingi na sekondari zimeanza kutolewa bure kitendo ambacho
maskini na wanyonge wa nchi hii wameanza kuuona mwanga.
Alisema ataendelea kumwombea
Magufuli kwa sababu kazi anazozifanya zinawanufaisha wanyonge na maskini ambao
kwa muda mrefu walipuuzwa katika nchi yao.
“Kuchaguliwa kwake kuwa mwenyekiti
ni zawadi kwetu Watanzania, tuendelee kumwombea kila siku ili aendelee kufanya
kazi yake kwa ufanisi zaidi,” alisema.
Alisema nafasi hiyo mpya
itamwezesha kupambana na rushwa tatizo ambalo ameonyesha kuwa `atalivalia
njuga’ hata ndani ya chama hicho.
Mbali na Rais Magufuli, Gwajima
aliwaombea pia Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, mawaziri na Spika wa Bunge kwamba
Mungu awalinde ili wamsaidie Rais kutekeleza majukumu yake.
Kwa mwezi mzima, Askofu Gwajima
amekuwa akitafutwa na Polisi baada ya kusambaa kwa sauti inayosikika kama yake
ikitaka Rais mstaafu Kikwete afikishwe mahakamani kwa makosa yote yaliyofanyika
katika utawala wake.
Katika mkanda huo, sauti hiyo
inadai baadhi ya viongozi wa CCM wametuma watu mikoani kupiga kampeni ya kutaka
Magufuli asipewe uenyekiti ambao umekuwa ukishikiliwa na Kikwete.
Baada ya sauti hiyo, Gwajima
aliondoka nchini kwenda Japan lakini Polisi waliendelea kumsaka hadi Julai 12
walipomkamata katika Uwanja wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA), aliporejea.
Alihojiwa na kuachiwa siku hiyohiyo.

No comments:
Post a Comment