
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema uamuzi wa Serikali kuhamia
siyo siasa kama watu wanavyodhani bali ni utekelezaji wa maamuzi kamili na
kwamba Serikali inakamilisha eneo la kisheria juu ya uamuzi huo.
“Hapa tulipofika ni hatua ya utekelezaji wa pamoja na hakuna
namna nyingine kwa sababu uamuzi umeshatolewa. Nataka niwahakikishie kwamba hii
siyo siasa, tunachokamilisha ni eneo dogo tu la kisheria juu ya uhamishaji wa
makao makuu kuja Dodoma na katika Bunge la Septemba sheria hii itapitishwa,”
amesema.
Ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumanne, Julai 26, 2016) wakati
akizungumza na viongozi wa mkoa, Serikali za mitaa, viongozi wa dini,
wajasiriamali, wazee wa mji huo, wasafirishaji, wafanyabiashara, wakuu wa
taasisi za elimu, za kifedha na watoa huduma mbalimbali katika mkutano
uliofanyika kwenye ukumbi wa Hazina ndogo mjini Dodoma.
Waziri mkuu ambaye aliitisha kikao cha kazi na wadau hao mjini
Dodoma, ameutaka uongozi wa mkoa huo pamoja na wadau wake wakae na kuandaa
mpango kazi wa jinsi ya kupokea na kutekeleza uamuzi wa Serikali kuhamia
Dodoma.
Pia ametoa siku 14 kwa uongozi wa mkoa wa Dodoma kukamilisha
mpango kazi wao na kumkabidhi mapendekezo yao ili yaweze kuingizwa kwenye
mpango mkubwa wa Serikali kuu.
“Uongozi wa Mkoa, ukishirikiana na Ofisi yangu kupitia Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Rais TAMISEMI usimamie na kuyaratibu
majukumu haya. Ndani ya siku 14 nipate proposal ya kwanza namna
mtakavyoyatekeleza. Naagiza kiundwe kikosi kazi chini yenu kitakachowajumuisha
makundi yote niliyoyataja,” amesema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu amesema chimbuko la uamuzi wa kuhamia Dodoma
kuifanya makao makuu ya Serikali lilikuwa ni ndoto ya Baba wa Taifa, Mwl.
Julius Kambarage Nyerere ambayo imeendelea kudumu katika Ilani ya Uchaguzi ya
Chama cha Mapinduzi ikiwemo Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2015 chini ya Ibara ya
151.
“Napenda kumshukuru Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu
Hassan, na viongozi wengine wote wa Chama kwa kusimamia ndoto ya
Baba wa Taifa ya kuhamishia Makao Makuu hapa Dodoma. Ni imani yangu kuwa
wananchi wote mtaunga mkono uamuzi huu muhimu kwa Serikali yetu na wananchi kwa
ujumla, amesema.
Akiweka msisitizo juu ya kazi kubwa inayowakabili viongozi hao,
Waziri Mkuu amesema masuala yanayotakiwa kufanyika kuanzia sasa ni pamoja na
Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) kuhakikisha eneo la makazi ya Serikali
Kuu litakalotumika kwa ofisi za wizara na taasisi zake, makazi ya watumishi na
huduma za biashara elimu na taratibu zote za kisheria za kulitwaa zinakamilika
kwa haraka na linakuwa tayari kwa matumizi.
“Natambua kazi iliyopo mbele yetu ni kubwa na inahitaji jitihada
za pamoja. Hivyo kila taasisi na mtu mmoja mmoja ana jukumu la kuhakikisha kuwa
tunajipanga vizuri na kuweka mazingira ya ujio wa Serikali katika maeneo yote
muhimu,” amesema.
Amezitaka Mamlaka za Mipango Miji na hasa CDA wahakikishe
wanaweka mfumo mmoja wa upatikanaji wa viwanja ambao utajulikana na kila mmoja,
utakuwa wazi usio na urasimu. “Mfumo huu wa viwanja uwekwe kwenye mfumo wa
kompyuta na uuzaji wa viwanja hivyo uwe wa kieletroniki kuepusha udanganyifu
kutoka kwa madalali,” amesisitiza.
Waziri Mkuu ameonya CDA na Manispaa zisibadili ramani ya mipango
miji iliyokwishawekwa awali kama vile maeneo ya wazi kutumika tofauti na
makusudio yaliyokusudiwa na akaagiza maeneo hayo yote yarejeshwe na kufufuliwa.
“Natambua katika makazi hapa Dodoma kulitengwa maeneo ya vituo
maalum vijulikanavyo kama D Centers kwa ajili ya kutoa huduma mbalimbali. Cha
ajabu sasa kuna magenge, groceries na sasa naagiza kwa hadhi ya Makao Makuu
haya maeneo sasa yatumike kuwekeza maduka makubwa (shopping malls) ambamo
huduma zote mbalimbali hupatikana,” amesema.
Ameitaka Manispaa iboresha usafi wa mazingira na bustani zake
kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali kuzitunza. Pia ameitaka manispaa ya mji
huo ishirikiane na TANROADS kuboresha barabara zote za mitaa na taa za
barabarani mji ukae kisasa, na usalama uwe bora zaidi.
“Eneo jingine muhimu ni Manispaa na CDA kuhamisha makundi
mbalimbali ya wafanyabiasahra na huduma za masoko yasiyo rasmi na kuyapa maeneo
yaliyo rasmi na bora zaidi. Hii ni pamoja na maeneo ya maegesho ya
bajaji, bodaboda, taxi na daladala. Pia mazingira ya Stendi Kuu yaboreshwe,
vyoo vya kulipia pia vijengwe katikati ya mji,” amesisitiza.
Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa Wakala wa majengo (TBA)
waorodheshe majengo yote ya Serikali na taasisi zake yanayotumika kwa sasa na
yasiyotumika, “Nataka muyawekee utaratibu maalum wa matumizi yake ili tupate
kujua yanayoweza kutumika kwa muda kwa baadhi ya wizara na taasisi zake. Hii ni
pamoja na jengo jipya la Mkuu wa Mkoa, linaloendelea kujengwa.”
Amewataka wakazi wa Dodoma watumie fursa hiyo kujenga nyumba za
kuishi za kutosha, nyumba za kulala wageni na mahoteli ili watu watumishi na
wageni wanapokuja wasipate taabu mahali pa kuishi.

No comments:
Post a Comment