
MAWAKILI wa kujitegema zaidi ya 100
mkoani Arusha, jana waliandamana kwenda kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha,
Charles Mkumbo, kulaani kile walichokiita ukandamizwaji wa sheria za nchi na
kazi ya uwakili unaofanywa na polisi.
Wanasheria hao wanalaani kitendo
cha wakili mwenzao, Shilinde Ngalula, kukamatwa, kufungwa pingu na kufunguliwa
mashtaka akiwa kazini Loliondo wilayani Ngorogoro.
Mawakili hao walitembea zaidi ya
hatua 400 kabla ya kuzingirwa na polisi ambao waliwataka kuunda kamati ya watu
wachache kwenda kuzungumza na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Charles
Mkumbo.
Uamuzi wa kufanya maandamano hayo,
ulipitishwa jana mjini hapa baada ya mawakili hao kufanya kikao cha pamoja
viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.
Awali, mawakili hao wakiongozwa na
Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Wakili Modest Akida, pia
walikubaliana kutoendelea na kesi za wateja wao waliokuwa mahakamani.
Akizungumzia maandamano hayo, Akida
alisema yalilenga kupinga kitendo cha Jeshi la Polisi wilayani Ngorongoro,
kumkamata na kumfungulia mashitaka Wakili Ngalula.
Wakiwa tayari wameandamana umbali
wa takribani hatua 400 kutoka mahakamani hapo, vikosi vya askari polisi
waliovalia kiraia na wale wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wakiwa ndani ya
magari mawili, waliwazunguka na kuwaamuru kusimama.
Mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi
Arusha, Thomas Mareko, aliwataka wanasheria hao kufuata sheria katika kudai na
kuwasilisha malalamiko yao.
“Nyinyi ni wanasheria, mpaka hapa
tayari mmeshaandamana kinyume cha sheria za nchi, nawaomba chagueni wawakilishi
nitawasindikiza mnakokwenda na wengine rudini mkaendelee na majukumu yenu,”alisema Mareko.
Baada ya maandamano hayo kuzuiwa,
mawakili hao waliwachagua wawakilishi waliokwenda kuwasilisha malalamiko yao
kwa Kamanda Mkumbo na wengine walirudi katika viwanja vya mahakama kusubiri
taarifa.
Awali, akizungumza katika viwanja
hivyo, Wakili George Njooka alisema mawakili nchini wameanza kudharauliwa na
vyombo vya dola.
“Hawa watu walianza na vyombo vya
habari, wakaenda kwa wanasiasa na sasa wamekuja kwa mawakili, nawaomba tuanzie
hapa twende kwa RPC atuambie haya maelekezo tunayoambiwa yanatoka juu, yanatoka
kwa nani,” alisema Wakili Njooka.
Wakili Qamara Peter aliwakumbusha
mawakili wenzake kuwa haki siku zote haiombwi bali inadaiwa.

No comments:
Post a Comment