
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 26 Julai, 2016 amekutana na kufanya
mazungumzo na Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt.
Frannie Leautier katika Ikulu ya Chamwino Mkoani Dodoma, ambapo ameishukuru
benki hiyo kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya Tanzania hususani
kutoa mikopo iliyowezesha ujenzi mkubwa wa barabara.
Pamoja na kuishukuru AfDB Rais
Magufuli ameiomba benki hiyo kuendelea kushirikiana na Tanzania katika
utekelezaji wa mipango na miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo mpango mkubwa
wa uzalishaji wa nishati ya umeme utakaofanikisha ujenzi wa viwanda, ujenzi wa
barabara zinazounganisha ndani na nje ya Tanzania na kuunga mkono juhudi za
kukabiliana na rushwa.
Kwa upande wake Makamu wa Rais wa
AfDB Dkt. Frannie Leautier amempongeza Rais Magufuli kwa juhudi kubwa
alizozianza katika kujenga uchumi wa Tanzania, kukabiliana na rushwa na
kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya serikali na ameahidi kuwa benki hiyo
itaendelea kuunga mkono juhudi hizo kwa kutoa mikopo ya masharti nafuu
itakayofanikisha mipango na miradi mbalimbali ya Tanzania.
"Tanzania ni nchi ambayo
inapata fedha kuliko nchi zote za Afrika katika mpango wa AfDB kupitia Mfuko wa
Maendeleo wa Afrika, hizi ni fedha ambazo zinatolewa kwa mkopo nafuu
zaidi kuliko mikopo mingine" Amesema Dkt. Frannie Leautier.
Dkt. Frannier Leautier amebainisha
kuwa AfDB inatarajia kuwa Tanzania itanufaika kupitia vipaumbele vitano vya
benki hiyo ambavyo ni kusaidia uzalishaji wa nishati, utangamano wa bara la
Afrika, maendeleo ya viwanda, usalama wa chakula na kuboresha hali ya maisha.
Aidha, Makamu wa Rais huyo wa AfDB
amesema kuanzia mwakani benki hiyo imepitisha miradi mikubwa mitatu kwa ajili
ya Tanzania ambayo ujenzi wa nyumba ya makazi, utoaji wa mikopo vijijini kwa
ajili ya kuendeleza kilimo na maeneo ya uchumi kupitia benki ya CRDB na kukiendeleza
Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Nelson Mandela kilichopo Arusha ambapo benki hiyo
itatoa Dola za Marekani Milioni 4.
Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na
Mwakilishi Mkazi wa AfDB Dkt. Tonia Kandiero, Naibu Waziri wa Fedha na
Mipango Dkt. Ashatu Kijaji.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dodoma
26 Julai, 2016

No comments:
Post a Comment