
BARAZA la Vijana la Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA) limeendeleza msimamo wake wa kuzuia Mkutano
Mkuu Maalum wa CCM, uliopangwa kufanyika Julai 23, mwaka huu mjini Dodoma.
Katika kuhakikisha linatimiza azma
yake hiyo, baraza hilo limesema wanachama wake wapatao 4,000 wamejiandaa kushiriki
kwenye shughuli hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari
jijini Dar es Salaam jana, baada ya kuhojiwa kwenye Kituo Kikuu cha Polisi,
Makamu Mwenyekiti wa Bavicha, Patrick ole Sosopi, alisema kuna vijana
watakaotoka sehemu mbalimbali ili kuzuia mkutano wa CCM.
Sosopi alisema Bavicha watakwenda
Dodoma kuzuia Mkutano Mkuu Maalum wa CCM kwa kile walichodai kusaidia Jeshi la
Polisi kutekeleza amri yake ya kuzuia mikutano ya kisiasa hadi 2020.
Alisema pia kuna watu wamejitolea
kutoa magari kwa ajili ya kuwabeba vijana hao ili kuwafikisha Dodoma kuunga
mkono agizo la polisi.
Sosopi pia aliomba Jeshi la Polisi
kuwachukulia hatua viongozi wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) kutokana na kauli
zao za vitisho walizozitoa dhidi ya Bavicha hivi karibuni.
Akizungumza na waandishi wa habari
Julai 4, mwaka huu, Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamad Shaka, aliionya Bavicha
wasiende Dodoma kuzuia Mkutano Mkuu Maalum wa CCM kwa kuwa watatumia kila mbinu
kuwazuia ili kulinda heshima ya chama chao.
Sosopi alisema wao hawataki
matatizo wala vurugu bali wanachofanya ni kutii agizo la polisi kwa unyenyekevu.
"Mkuki kwa nguruwe kwa
binadamu mchungu kwani Rais alipopiga marufuku mikutano ya kisiasa hadi 2020,
CCM walichekelea wakiamini kuwa Chadema tumekomolewa lakini iweje sasa Jeshi la
Polisi likubali kuruhusu mkutano wao wakati Chadema hata mikutano ya ndani
tunazuiliwa?
"Hatutanii hata kidogo na wala
CCM wasidhani kuwa hatutakwenda Dodoma lakini tunaliomba Jeshi la Polisi
litende haki juu ya kauli za uchochezi kwani nilitegemea viongozi wa UVCCM
wangekamatwa na jeshi hilo lakini tunaokamatwa ni sisi tu," alisema Ole
Sosopi.
Akizungumzia suala la kuhojiwa na
polisi jana, Ole Sosopi alisema alikuwa kituoni hapo kuhojiwa kwa kosa
analodaiwa kufanya Juni 18, mwaka huu la kutoa kauli za uchochezi.
Sosopi alikamatwa mara ya kwanza
Juni 26, mwaka huu mkoani Iringa na kusafirishwa hadi jijini Dar es Salaam na
kuhojiwa kwa kosa hilo katika
shughuli ya mahafali ya wanachama wa Chadema waliomaliza vyuo vikuu.
Sosopi alisema baada ya kuhojiwa
jana na polisi, anatakiwa kuripoti tena kituoni hapo Julai 18, mwaka huu.
Akizungumzia suala la Sosopi,
mwanasheria wake, Frederick Kihwelo alisema Sosopi aliripoti kituoni hapo kwani
anakabiliwa na tuhuma ya kutoa lugha ya uchochezi.
Alidai lengo la mteja wake ni
kuhakikisha polisi wanatenda haki bila upendeleo kwani kazi yao kubwa ni
kulinda usalama wa raia na mali zao
Alisema baada ya kuhojiwa na polisi
jana, atatakiwa kufika tena kituoni hapo Julai 18, mwaka huu wakati huu
upelelezi unafanyika na ushahidi kupelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaki ya Jinai
(DPP) ili aamue kama kuna kesi ya kujibu au la.

No comments:
Post a Comment