
Rais John Magufuli amemwaga
burungutu la fedha kusaidia Waislamu ambao watakwenda kuhiji Agosti mwaka
huu.
“Najua kuna Waislamu watakwenda
kuhiji nadhani Agosti, naomba kama inaruhusiwa na mimi nichangie kitu kidogo
kadri ya uwezo wangu, nimejipigapiga na mimi nikaona nichangie kitu kidogo,
kana inaruhusiwa naomba Mufti uje nikukabidhi,” alisema
Magufuli alipokuwa akizungumza katika Baraza la Eid el Fitri jijini Dar es
Salaam jana.
Baada ya kutamka maneno hayo,
alishika begi dogo kama briefcase akampa msaidizi wake ambaye alilifungua na
kuchomoa burunguti la noti na kumkabidhi Mufti, Sheikh Mkuu Zubeiry Ally.
Hata hivyo haikufahamika kiasi cha
fedha hizo. Kabla ya kutoa fedha hizo, awali akimkaribisha Rais Magufuli
kuhutubia, Mufti Zubeiry aliwataka Waislamu kutumia Bakwata katika safari za
hija zitakazogharimu Dola 3,800 kwa mtu mmoja.
Awali Magufuli alikuwa ameahidi
kitita cha Sh2 milioni kwa kijana aliyesoma dua katika sherehe hizo pamoja na
kiasi kingine kama hicho kwa kundi la Kaswida lililotumbuiza.
Katika hotuba yake, Dk Magufuli
alisema Serikali yake ipo katika mchakato wa kurejesha heshima yake ingawa kuna
watu wachache watakaoguswa kwa kuisababishia hasara Serikali.
Rais Magufuli aliyekuwa mgeni rasmi
katika baraza hilo la Eid el Firti alisema Tanzania ni nchi tajiri lakini
baadhi ya watu wamesababisha watu waendelee kuwa masikini.
“Tanzania hii ni tajiri sana, kila
kitu kipo. Juzi mpaka wamegundua Helium tani za kutosha. Kila madini yapo hapa.
Lakini kwa nini tuko masikini? Kwa nini watu wana shida? Ndiyo maana tumeamua
kwa niaba yenu turudishe heshima yetu. tulete mabadiliko ya kweli na katika
kufanya hayo wapo watu watakaoguswa, lakini ni wachache sana kuliko wale
waliokuwa wanaguswa kwa kuibiwa, ni wachache waliokuwa wanadhulumiwa,” alisema Rais
Magufuli.
Alisema kwa miezi saba tangu
alipochaguliwa kuingia madarakani Serikali yake imetekeleza mambo kadhaa ikiwa
pamoja na kutoa elimu bure kwa shule za msingi na sekondari, kurudisha nidhamu
ya watumishi wa umma, kudhibiti matumizi mabaya ndani ya Serikali, kuongeza
mapato na mengineyo.
“Pamoja na hatua hizo ni dhahiri
kuwa bado tuna safari ndefu katika kutimiza yale tuliyokusudia na tuliyowaahidi
Watanzania. Naomba niwahakikishie kwamba dhamira ya kuwahudumia kwa nguvu
zetu zote pamoja na vipaji vyote bado tunayo. Tuna sababu ya msingi na tuna
imani kuwa Mungu yupo kuhakikisha kuwa tunaipeleka nchi yeti mbele...” alisema Rais
Magufuli huku akiwataka waumini hao kuiombea Serikali.
Aliwataka viongozi wa dini ya
Kiislamu kuwahimiza waumini wao kushiriki katika shughuli za maendeleo hususani
katika kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano ambao utekelezaji wake
umeanza mwezi huu.
“Tusipofanya kazi hatutapata pesa.
Ndiyo maana wale waliozoea kupata fedha za bure wameanza kusema fedha zimeisha
mifukoni. Hela haiji bila kufanya kazi,” alisema.
Kuhusu mali za Waislamu
zilizodhulumiwa, Rais Magufuli alisema atawasaidia kuzirejesha.
Alimpongeza Mufti wa Baraza la
Waislamu Tanzania (Bakwata), Zubeiry akisema alikuwa mstari wa mbele katika
kurejesha mali hizo kabla hata hajapewa cheo hicho.
“Nakumbuka wakati nikiwa Waziri wa
Ardhi, kabla hujawa Mufti, pamoja na viongozi wa Bakwata na wengine, ulifika
ofisini kwangu ukieleza jinsi mali za Waislamu zilivyokuwa zinadhulumiwa.
"Ninafamu pamekuwa na hiyo
tabia ya baadhi ya viongozi wenye mali kuwatumia viongozi wa Bakwata na dini
nyingine katika kuwarubuni na kuingia ubia, mali hizo baadaye huwa zinapotea
kabisa,” alisema na kuongeza:
“Tujitahidi kwa nguvu zote
kusimamia mali hizi, zisije kuwa chanzo cha kuvunjika kwa amani. Tunapenda
wawekezaji lakini wanachokiahidi hawatekelezi, haiwezekani.
"Haiwezekani na wala
haikubaliki kwa watu kwa ujanja wao na wakati mwingine kwa kutumia wanasheria
wao kukalia mali za Waislamu. Mali za Waislamu lazima zirudi na za Wakristo
zirudi ili amani iwepo.”
Baraza hilo lilihudhuriwa na Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa, Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Paul Makonda, Katibu wa Bakwata Sheikh Suleiman Lolila na mabalozi wa
nchi mbalimbali na waumini wa dini hiyo.

No comments:
Post a Comment