
KIONGOZI wa Kanisa la Ufufuo na
Uzima, Askofu Josephat Gwajima, amefunguka kwa kuelezea safari yake aliyoifanya
nje ya nchi hivi karibuni, baada ya taarifa mbalimbali kudai kuwa alilikimbia
Jeshi la Polisi.
Akiongoza ibada kanisani kwake,
Ubungo, jijini Dar es Salaam jana, Askofu Gwajima alisema aliondoka nchini
kwenda Japan Juni 15, mwaka huu, kwa ndege ya Emirates.
Akitoa mahubiri katika ibada jana,
Gwajima alisema alifika mjini Osaka Juni 16 na kuanza mkutano wa kuhubiri
injili na siku zilizofuata alikwenda katika miji mbalimbali.
Askofu Gwajima ambaye aliingia
kanisani hapo saa 5:00 asubuhi na kuanza kuhubiri dakika 15 baadaye, asubuhi
alitumia muda wa saa tatu hadi saa 8:20 kumaliza mahubiri yake.
Baada ya kuanza kuhubiri, alielezea
safari hiyo kwa kutaja miji aliyekwenda ikiwamo Nagoya alikohubiri kwa siku
mbili, Karuizawa, Ibaraki, Hiloshima na Yanakochi.
“Safari yangu ilikuwa ya mafanikio
sana. Tulisafiri salama na kuzunguka miji mbalimbali na tulirudi Jumatatu ya
wiki iliyopita,” alisema Askofu Gwajima.
Kadhalika, katika mahubiri hayo,
Gwajima aliwakumbusha waumini wa kanisa hilo kuhusu kuhama kwa kanisa hilo, kwa
kuwatajia siku ya mwisho ya kumalizia michango kwa ajili ya ujenzi wa kanisa
jipya kuwa ni Julai 30, bila ya kutaja sehemu ambayo kanisa hilo litahamia.
Hata hivyo, Askofu Gwajima wakati
wote wa mahubiri, hakuzungumzia suala la kuhojiwa kwake na Jeshi la Polisi.
Wakati huo huo, mwandishi
alizungumza na Msaidizi wa Askofu Gwajima, Yekonia Bihagaze, kuhusu tetesi
za kufungiwa kwa kanisa hilo na kusema taarifa hizo si za kweli bali ni maneno
ya mitaani.
“Hayo maneno si ya kweli. Si umeona
ibada imeendelea kama kawaida na Askofu amehubiri? Maneno ya mtaani usiyalete
kanisani,” alisema Bihagaze.
Julai 12, mwaka huu, Kikosi cha
Polisi cha Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA) kilimkamata Askofu Gwajima
wakati akitokea Japan kwa kutumia ndege ya Shirika la Ndege la Kenya.
Baada ya kukamatwa, alipelekwa moja
kwa moja Kituo Kikuu cha Polisi kwa ajili ya kuhojiwa, akidaiwa alitoa maneno
ya uchochezi mwezi uliopita.
Jeshi la Polisi lilikuwa
likimtafuta Askofu Gwajima baada ya kusambazwa mkanda kwenye mitandao ya
kijamii unaodhaniwa una sauti yake.
Katika mkanda huo, Gwajima
anapendekeza Rais mstaafu Jakaya Kikwete afikishwe mahakamani kwa yote
yaliyofanyika wakati wa utawala wake, ambayo kwa sasa Rais Magufuli
anayashughulika kwa staili ya utumbuaji majipu.
Pia Gwajima alisikika akimshauri
Rais John Magufuli, kuhama Chama Cha Mapinduzi (CCM) iwapo watakataa kumkabidhi
uenyekiti na kwamba apeleke muswada bungeni, kuondoa kinga ili rais ashtakiwe
kwa makosa aliyoyafanya akiwa madarakani.
Tangu kusambaa kwa mkanda huo,
Jeshi la Polisi lilikuwa likipiga kambi katika moja ya nyumba za Askofu
Gwajima, iliyoko Mbezi Salasala jijini Dar es Salaam.
Pamoja na kupiga kambi, jeshi hilo
halikufanikiwa kumkamata na baadaye ilielezwa kuwa amekwenda nje ya nchi
kuhubiri.

No comments:
Post a Comment