
Siku chache baada ya Mkuu wa Mkoa
wa Dar es Salaam Paul Makonda kutoa agizo la msako wa nyumba hadi nyumba ili
kuwabaini watu wasio na kazi maalum, Meya wa Jiji la Dar es Salaam Isaya Mwita
aliibuka na kudai agizo hilo ni batili na haliwezi kutekelezeka kwa mujibu wa
sheria, kanuni na taratibu za nchi.
Jukwaa Huru la Wazalendo kwa Mkoa
wa Dar es Salaam kupitia kwa Mwenyekiti wake Andrew Kadege wamelaani vikali
kitendo kilichofanywa na Meya wa Dar es Salaam, Isaya Mwita kwa kufanya
harakati za siasa badala ya zile za kuwaletea wananchi maendeleo huku akiwapotosha
kwa makusudi wananchi na kuwataka kukaidi agizo la Makonda.
Jukwaa Huru la Wazalendo Tanzania
limewataka wananchi wa Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla kutoa ushirikiano
mara zoezi la kuwatambua wakazi katika kaya litakapoanza rasmi ili kupata
takwimu sahihi kwa maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla hususan
katika kipindi hiki ambapo serikali inataka kuanza ugawaji wa Sh. Milioni 50
kusaidia maendeleo ya kaya.
Hata hivyo jukwaa limemtaka meya
kutokuendelea na tabia ya kuwalaghai wanainchi kutoshiriki katika shughuli za
maendeleo kwani ndio sehemu yao ya kujikwamua kiuchumi na kuondoa
umasikini unaowakabili watanzania kwa ujumla.
Jukwaa limeongeza kuwa hatua
hiyo ya mkuu wa mkoa wa Dar es salaam ya kutaka kuwatambua
wanainchi wa mkoa wake wa Dar es salaam katika ngazi ya kaya ni
kutaka kujua jinsi gani ya kuweza kupanga na kuwahudumia kama
ilivyo katika majiji ya London,Paris na Berlin inavyofanyika.
Jukwaa huru limechukua nafasi hiyo
kuwaomba na kuwashauri wanainchi wote popote litakapo fanyika zoezi
hilo kushirikiana na serikali kikamilifu kwani ni kwa manufaa ya
wanainchi wenyewe na taifa kwa ujumla ili kuweza kuinua uchumi.

No comments:
Post a Comment