
JESHI la Polisi Kikosi cha Usalama
Barabarani nchini kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi
Kavu na Majini (SUMATRA) imesitisha leseni za madereva 18 kutokana na mgomo
walioufanya kupinga wenzao kupelekwa mahakamani.
Wamiliki wa mabasi 12 ambayo
madereva hao walikuwa wanaendesha kwenda sehemu mbalimbali nchini, wamepewa
siku saba kujieleza ni kwa nini wasifutiwe leseni za kutolea huduma hizo pamoja
na kutakiwa kusitisha ajira kwa madereva hao.
Akizungumza na waandishi wa habari
jana Dar es Salaam, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga,
alisema Julai 23 mwaka huu mkoani Kagera, madereva wa mabasi hayo walifanya
mgomo kupinga kitendo cha madereva wenzao kupelekwa mahakamani, kukosa dhamana
na kulala rumande kutokana na makosa mbalimbali ya usalama barabarani ikiwamo
kuendesha kwa mwendo kasi.
Kamanda Mpinga alisema dereva
yeyote atakayeendesha gari kwa kasi ya zaidi ya kilometa 90 kwa saa atafikishwa
mahakamani na sio kutozwa faini kama awali ili kuhakikisha matukio ya ajali
yanapungua nchini.
Alisema kutokana na hali hiyo
madereva wanaoendesha mabasi yanayoanza safari zake kwenye Manispaa ya Bukoba,
walisitisha huduma kwa kushinikiza Mahakama iwaachie wenzao waliokamatwa kwa
makosa ya mwendo kasi.
‘’Serikali haitavumilia kuona
madereva wasiofuata sheria za usalama barabarani na sheria za kazi na ajira.
Jeshi la Polisi ndio tunawapa madereva mafunzo, tunasajili vituo vya mafunzo na
kuwapa leseni. Hivyo tunasitisha leseni zao kwa mujibu wa sheria kwa kukiuka
kanuni za leseni,’’ alisema Mpinga na kuongeza kuwa askari watakaoachia
madereva na kampuni za mabasi kutembea kwa zaidi ya kilometa 90 kwa saa
watachukuliwa hatua za kinidhamu.
Mkurugenzi wa Sumatra, Gilliard
Ngewe, aliyataja mabasi pamoja na madereva waliositishiwa leseni kuwa ni
Hussein Tegatega na Miraji Kondo wa Kampuni ya RS Express wanaoendesha basi
lenye namba za usajili T 425 DDT aina ya Zongtong linalotoka Bukoba kwenda Dar
es Salaam.
Said Omary na Amos Danney wa basi
la Kimotico lenye namba za usajili T 966 CDY aina ya Nissan linalotoka Bukoba
kwenda Arusha na madereva wanne wa mabasi ya Princess Muro yenye namba za
usajili T 166 DCA na T 923 DCT yanayosafiri kutoka Bukoba kwenda Dar es Salaam.
Madereva hao ni Ally Mshuza,
Twalibu Ondossy, Costa Andrew na Witness Lema.
Madereva wengine ni Musa Tindwa na
Gerald Beti wa Kampuni ya Osaka Raha wanaoendesha basi lenye namba za usajili T
968 CPC linalofanya safari zake Bukoba kwenda Dar es Salaam na Paul Ngussa wa
basi lenye namba za usajili T 810 BDW aina ya Scania linalotoka Bukoba kwenda
Musoma, mali ya Kampuni ya Bunda Express.

No comments:
Post a Comment