
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Iringa
imemtia hatiani askari Polisi, Pacificius Cleophace Simoni, kwa kosa la mauaji
ya bila kukusudia ya mwanahabari Daudi Mwangosi yaliyotokea Septemba 2 mwaka
2012 katika kijiji cha Nyololo wilayani Mufindi mkoani Iringa.
Kwa mara ya kwanza Simoni
alifikishwa mahakamani hapo Septemba 12 mwaka 2012 akituhumiwa kufanya kwa
kukusudia mauaji hayo wakati mwandishi huyo alipokuwa akiwajibika katika kazi
zake za kutafuta habari kwenye ufunguzi wa matawi ya Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema).
Ushahidi uliowasilishwa mahakamani
hapo na upande wa Jamhuri umeilazimisha mahakama hiyo chini ya Jaji Kihwelo
kuibadili kesi hiyo kutoka kwenye mauaji ya kukusudia na kuwa mauaji ya bila
kukusudia ambayo hukumu yake ameisogeza mbele hadi kesho Jumatano.
Baada ya mabadiliko hayo, wakili wa
upande wa Jamhuri, Adolph Maganga, aliiomba mahakama hiyo imhukumu mtuhumiwa
huyo kifungo cha maisha jela kwa mujibu wa Kifungu cha 198 cha Sheria ya Kanuni
ya Adhabu huku wakili wa utetezi, Lwezaula Kaijage akiiomba mahakama hiyo
impunguzie adhabu kwa kumfunga kifungo cha nje.
Wakati akitetea hoja yake ya
kuiomba Mahakama itoe adhabu ndogo ya kifungo cha nje kwa mtuhumiwa huyo,
Lwezaula aliisihi mahakama hiyo imuonee huruma mtuhumiwa huyo kwa kosa
alilolifanya bila kukusudia kwa sababu ni kijana mdogo mwenye miaka 27
anayetegemewa na Taifa kama nguvu kazi.
“Na alishiriki operesheni
iliyosababisha maafa hayo bila ridhaa yake, amekaa mahabusu kwa miaka minne na
katika kipindi hicho atakuwa amejutia sana kosa lake, amefiwa na wazazi wake
wote wawili, ana wadogo zake watano wanaomtegemea na ana mke na mtoto mmoja
mdogo,” alisema wakili
huyo wakati akitoa ombi hilo.
Kwa msingi huo, wakili huyo
alitumia Kifungu cha 38(11) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 kuomba
Mahakama imhurumie mtuhumiwa huyo na kumfunga kifungo cha nje.
Akisoma maelezo ya kesi hiyo kabla
ya kuibadili na kuwa na mauaji ya bila kukusudia, Jaji Kiwehlo alisema upande
wa Jamhuri ulileta mashahidi wanne ambao kati yao watatu walitoa ushahidi
ulioshindwa kuithibitishia moja kwa moja Mahakama kama mtuhumiwa huyo
alikusudia alipofanya mauaji hayo.
Huku akishangaa kwa nini Jamhuri
pamoja na kuwa na rasilimali za kutosha ilishindwa kuwaleta mashahidi wengine
muhimu kama Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa wa wakati huo, Michael
Kamuhanda na Ofisa Upelelezi wa Mkoa Wankyo, aliwataja mashahidi hao kuwa ni
Said Mnuka, Azel Mwampamba na Lewis Obado ambao pia wote walikuwa askari Polisi
wa vyeo tofauti.
Alisema ushahidi pekee uliomtia
hatiani mtuhumiwa huyo ni ushahidi uliotolewa na shahidi namba tatu ambaye ni
mlinzi wa amani, Flora Mhelela.
Mlinzi huyo wa amani aliwasilisha
mahakamani hapo ungamo la mtuhumiwa huyo lililomhusisha na mauaji hayo na
ambalo wakati likiwasilishwa upande wa utetezi haukulikana pamoja na kwamba
ulikuja kulikana baada ya ungamo hilo kuwasilishwa mahakamani hapo.
Kwa kupitia ungamo hilo ambalo
Mahakama imejiridhisha bila shaka yoyote kwamba maelezo yake yalitolewa kwa
hiari na mtuhumiwa huyo; mtuhumiwa huyo alikiri kuhusika na mauaji hayo
japokuwa alisema yalikuwa ni ya bahati mbaya.
Sehemu ya ungamo hilo lililosomwa
mahakamani hapo kwa mara nyingine tena na jaji huyo linasema; “Niliondoka kutoa msaada nikiwa na long range ambayo ni
silaha inayotumika kupigia mabomu ya kishindo na machozi kama inavyoonesha
katika gazeti la Mwananchi la Septemba 3, 2012.”
“Pale katika eneo la tukio bila
kujua wala kufikiria likafyatua bomu, likafunguka likamuua mwandishi Daudi
Mwangosi na kumjeruhi OCS ambaye alikumbatiwa na marehemu, pia kuwajeruhi
askari wengine watatu waliokuwa karibu yangu na marehemu.”
Watu mbalimbali walijitokeza
kusikiliza kesi hiyo ni pamoja na Rais wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania
(UTPC), Deo Nsokolo na Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF),
Deudatus Balile.
Wengine waliojitokeza kuhudhuria
kesi hiyo ni pamoja na wanaharakati wa haki za binadamu, wanahabari wa Mkoa wa
Iringa na wananchi wa Manispaa ya Iringa.

No comments:
Post a Comment