
JESHI la Polisi nchini, limesema
linafanya uchunguzi kubaini baadhi ya vijana wanaojiunga na vikundi vya
kigaidi, vikiwamo IS na Al-Shabaab ili wawachukulie hatua za kisheria.
Akizungumza na waandishi wa habari
Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI),
Diwani Athuman, alisema wimbi la vijana hao kujiunga na makundi hayo
yanayopigwa vita duniani kote, linatokana na ushawishi wa baadhi ya watu.
“Tuna taarifa za kuwapo baadhi ya
vijana wa Kitanzania wanaojiunga na vikundi vya ugaidi… suala hili ni la
kiintelijensia zaidi, hatuwezi kulizungumzia kiundani, tunaendelea kulifanyia
kazi, tutakapofikia sehemu nzuri tutawaambia,” alisema
Athuman.
Alisema wakati suala hilo
linaendelea kufanyiwa kazi, jeshi hilo liliendesha operesheni maalumu ya siku
mbili, ambayo ilishirikisha nchi 26 za Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.
Alizitaja nchi hizo kuwa ni
Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Angola, Botswana, Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Lesotho, Malawi, Madagascar, Mauritius, Msumbuji,
Namibia, Afrika Kusini, Swaziland, Zambia, Zimbabwe, Comoro, Djibouti, Eritrea,
Ethiopia, Shelisheli, Sudan Kusini na Somalia.
Alisema operesheni hiyo
iliyojulikana kama ‘Operesheni Usalama III’ ilishirikisha nchi zaidi ya 26 na
ilisaidia kukaguliwa kwa magari 1,632 ambayo kati ya hayo, 10 yalikuwa ya wizi
huku matano yalibainika yameingiliwa ‘chases’.
Alisema operesheni hiyo pia
ilisaidia kukamatwa pikipiki 12 za wizi, huku 18 zikiendelea kufanyiwa
uchunguzi zaidi kutokana na kutokuwa na vibali halali.
Athuman alisema operesheni hiyo
ilisaidia pia kukamatwa aina mbalimbali ya dawa za kulevya, zikiwamo heroine
gramu 83, bangi kilogramu 398.6, mirungi kilogramu 30, bunduki aina ya shotgun
moja, gobole 11, risasi 104, mkuki mmoja na vipande 15 aina ya exprojel v6,
cotex na detonator.
Alisema walikamata wahamiaji haramu
43 maeneo mbalimbali nchini, kati yao 18 ni raia wa DRC, ambao
walikamatwa mikoa ya Rukwa na Kagera, wakati 22 wanatoka Burundi waliokamatwa
mikoa ya Shinyanga, Tabora na Kagera na raia wawili wa Rwanda walikamatwa
Kagera na mmoja wa Kenya alikamatwa Tabora.
“Katika operesheni hii tulifanya
ukaguzi katika kampuni mbalimbali zinazofanya biashara ya madini ambapo tatu
zilionekana kukosa uhalali wa kupewa leseni ya kuendelea kufanya biashara ya
madini,
“Kampuni hizi ni Delicore Metal
Company Ltd, Madandwa Gold Mining Export Import (T) Ltd na Alex Mining Co. Ltd,
na tatizo lao linaendelea kushughulikiwa na Wizara ya Nishati na Madini. Pia
yalikamatwa madini aina ya Acquqmiline Smoky Quartz kilogramu 20.
Alisema pia walikamata gamba moja
la kasa mkoani Ruvuma, mbao 410 zilizokuwa zikisafirishwa bila kibali mikoa ya
Pwani, Iringa na Morogoro, nyama ya pundamilia kilo 45 na bidhaa bandia.

No comments:
Post a Comment