WATU watatu wakiwemo wanafunzi
wawili wa vyuo vikuu vilivyoko jijini Dar es Salaam wamepandishwa kizimbani
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na mashitaka
ya mauaji.
Wanafunzi hao ni wa Chuo Kikuu cha
Ardhi, Hussein Mustafa (26) na wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Haruna Nkuye (24) ambao
wanashitakiwa pamoja na fundi makenika Rajabu Ally (41) wote wakazi wa Dar es
Salaam.
Washitakiwa hao wanaodaiwa kuhusika
na mauaji hayo kwenye tukio la ujambazi katika Benki ya CRDB eneo la Chanika
Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, walisomewa mashitaka na Wakili wa Serikali
Jackson Chidunda mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shahidi.
Akisoma hati ya mashitaka, Chidunda
alidai Desemba 8, mwaka jana katika eneo la Chanika, Wilaya ya Ilala, Dar es
Salaam, washitakiwa walimuua Ramadhani Halili, Shan Rajabu na Thomas Otemu.
Hakimu Shahidi alisema washitakiwa
hawatakiwi kujibu mashitaka kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza
shauri hilo isipokuwa Mahakama Kuu.
Upande wa jamhuri ulidai kuwa
upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa ili
wamuunganishe mshtakiwa Mohamed Ungando ambaye jana hakuwepo mahakamani.
Awali, mshitakiwa Mustafa aliiomba
mahakama imsaidie apate matibabu kwa kuwa viungo vinamuuma kutokana na adhabu
alizopewa akiwa mahabusu.
Hakimu Shahidi alisema gerezani
kuna utaratibu wa matibabu, kama hatatibiwa kesi itakapotajwa tena aijulishe
mahakama. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Julai 14, mwaka huu.

No comments:
Post a Comment