SERIKALI imeiamuru Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA) kuzishikilia akaunti za Kampuni kubwa ya mafuta ya
Uingereza (BG Group) hadi pale itakapolipa Kodi ya Ongezeko la Mtaji (capital
gain tax) yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 502.
Taarifa zilizoandikwa na gazeti
moja la wiki, TRA tayari imetoa maelekezo kwa Benki ya Citi kushikilia akaunti
za kampuni hiyo.
TRA inadai kiasi hicho kutokana na
faida iliyotokana na BG Group kuziuza hisa zake asilimia 60 kwa kampuni
nyingine za nishati za Royal Dutch Shell, Exxon Mobil, Ophir Energy na Statoil.
Biashara hiyo, pia ilihusisha
maslahi ya BG, visima vya mafuta namba 1 na 4 vilivyopo kusini mwa Tanzania.
Vyanzo vya habari kutoka Wizara ya
Fedha na TRA, vilisema amri hiyo imetolewa kushikilia akaunti za BG Group hadi
kodi hiyo itakapolipwa.
Baada ya akaunti kukaguliwa,
ilibainika fedha zilizopo katika benki hiyo, ni Dola milioni 5 tu, ikiwa ni
sawa na asilimia moja tu ya kiasi inachodai TRA.
Uamuzi huo unazua maswali katika
rufaa, ambayo BG Group imeifungua katika Mahakama ya Kodi Tanzania
ikipinga namna tathimini ilivyofanyika kupata kiasi hicho inachodaiwa.
BG Group, inasema haiwezi kulipa
kodi kwa sababu iliwekeza Dola milioni 850 ya jumla ya faida iliyopata katika
visima Tanzania.
BG Group iliendelea kudai kampuni
yake dada, tayari imetumia dola bilioni 1.5 kama uwekezaji, na hivyo kuashiria
upotevu wa mtaji.
Kwa mujibu wa Sheria ya Rufaa ya Kodi
ya Mapato (2006), mtu yeyote asiyeridhishwa na kiasi cha kodi anachodaiwa
anaweza kupinga kwa kumuandikia Kamishina Mkuu.
Ibara ya 12 (3) ya sheria hiyo
inasema. “Wakati taarifa ya kupinga kiasi cha kodi kinachodaiwa
inapowasilishwa, mtu anayepinga anatakiwa wakati akisubiri uamuzi wa mwisho wa
Kamishina Mkuu kwa mujibu wa Ibara ya 13, alipe kiasi cha kodi ambacho
hakikupingwa au theluthi moja ya kiasi kilichopingwa, bila kujali ukubwa wa
kiwango”.
Lakini wanasheria na wataalamu wa
nishati, wameitaka Serikali na BG Group kutatua mkwamo huo, ambao unaweza
kuchelewesha uamuzi wa mwisho wa uwekezaji wa dola milioni 30 wa mradi wa
usindikaji wa gesi ya asili ya matumizi mbalimbali (LNG), ambao kampuni hiyo
ina mipango ya kuijenga kwa ubia na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania
(TPDC).
Ujenzi huo wa mtambo wa LNG,
utakaozalisha tani milioni 10 za gesi kwa mwaka, awali ulikuwa ukamilike mwaka
2020.
Lakini chini ya sheria za nchi,
ujenzi hauwezi kupitishwa hadi kodi itakapolipwa kwanza.
Serikali imebakia kimya kuhusu
suala hilo, lakini Kamishina Mkuu wa TRA, Alphayo Kidata alisema suala hilo
bado halijafika kwake, huku Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter
Muhongo akilitaka gazeti hilo kumuuliza Mkurugenzi Mkuu wa TPDC, Dk. James
Mataragio, ambaye hakuwa tayari kusema lolote.
Kuna wasiwasi mizozo kuhusu kodi
inaweza kuathiri uwekezaji wa kigeni unaotarajiwa kuwekezwa nchini.
Wachambuzi wa mambo wanaamini
kampuni ya Shell kupitia hisa BG, imejipanga kimkakati kujipatia vibali vya
utafutaji wa mafuta Zanzibar kwa sasa kwa vile inamiliki pamoja na Serikali.
Shell imekuwa ikihaha kwa miaka 10 sasa kujipatia vibali vya utafutaji mafuta
visiwani humo.
Subiro Mwapinga, mshauri katika
kampuni ya ushauri wa masuala ya gesi na mafuta ya Mnazi Bay Consulting Group,
alisema mzozo wa sasa wa kodi umeuweka uwekezaji wa LNG katika hatari na
unaweza kuathiri miradi mingine, ikiwamo ujenzi wa pipa la mafuta baina ya
Uganda hadi Tanga wenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 10.
“Iwapo ukokotoaji wa kodi wa TRA
umefanywa kwa kufuata taratibu zote za kimataifa na kuendana na sheria, kuna
nafasi ndogo kwa BG Group kuweza kukwepa kulipa kodi, lakini bado hilo lina
athari zake linapokuja suala la kubadilisha miundo ya mradi wa LNG, ambayo
imepangwa kujengwa kwa ubia na washirika mbalimbali.
Kwa mfano, linaweza kusababisha
washirika wengine kujenga miradi yao wenyewe ya LNG,” anasema Mwapinga.
Vyanzo vya habari ndani ya Wizara
ya Fedha na TRA vilisema serikali pia imeamua kwa muda kusimamisha maombi ya
Shell na BG Group ya kufufua vibali vya kutafiti nishati katika visima viwili
hadi mgogoro huo utakapomalizika.
Kibali cha kisima namba 1 kinaishia
Desemba mwaka huu, huku cha kisima namba 4 kikiishia Oktoba 2017.
Vibali vya kutafuta mafuta hutolewa
kwa kipindi cha miaka minne kisha kufufuliwa kwa miaka minne mingine na kisha
kipindi kingine cha miaka mitatu, baada ya hapo kampuni inatarajia kuomba
kibali cha uendelezaji.
Kisha kwa mujibu wa kumbukumbu za
serikali, kampuni itaongezewa wastani wa chini wa miaka 11 na kuomba vibali vya
maendeleo lakini haiko tayari bado kwa hilo.
“Hali hiyo inaonesha Shell inatakiwa
kuomba kuongezwa muda kwa kibali cha kutafuta mafuta kwa ajili ya kisima namba
1 na 4, lakini ongezo la muda huwa chini ya mamlaka ya waziri kwa vile
liko nje ya kipindi cha miaka 11. Ni hapo serikali ndiyo iliyoshikilia
mpini,” vyanzo vya habari vilisema.
Mbunge wa Karagwe, Innocent
Bashungwa (CCM) na mratibu wa zamani wa Taasisi ya Kuongeza Uwazi na
Uwajibikaji katika Tasnia ya Uziduaji Tanzania,alisema usimamizi wa sekta ya
mafuta na gesi unahusisha mabilioni ya dola za uwekezaji na miamala mbalimbali
katika shughuli za hapa na pale.
“Wakati kunapotokea mabadiliko,
migogoro inaweza kuibuka iwapo mfumo wa sheria wa nchi husika hauko wazi kuhusu
taratibu za miamala,” alisema Bashungwa.
Mbunge huyo alisema, migogoro ni
ishara ya udhaifu wa kisheria na maandalizi ya taratibu. “Naamini
Serikali na BG zitapata suluhu kwa amani kwa fedha hizo za ongezeko la mtaji
zinazobishaniwa.
“Vinginevyo wanachama wa Chama cha
Mafuta na Gesi Tanzania na wawekezaji watarajiwa watalichukulia kama kengele ya
hatari ya kitakachowatokea siku za usoni,” alisema mbunge
huyo.

No comments:
Post a Comment