
RAIS John Magufuli, amelishukia
Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na la Magereza kwa kutengeneza idadi ndogo ya
madawati kutokana na Sh. bilioni nne zilitolewa na Bunge la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Aprili, mwaka huu.
Akizungumza wakati wa shughuli ya
makabidhiano ya madawati hayo kwenye viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam
jana, Rais Magufuli alieleza kushangazwa kwake na majeshi hayo kutengeneza
madawati 53,450 tu katika kipindi cha miezi mitatu (siku 90) tangu fedha hizo
zilipotolewa wakati wana nguvu kazi ya kutosha.
Hata hivyo, taarifa iliyotolewa
jana jioni na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa, ilieleza
kuwa, madawati 61,385 ndiyo ambayo yametengenezwa katika awamu ya kwanza
kutokana na fedha hizo za Bunge, ikiwa ni idadi tofauti iliyosemwa na Rais
mapema kwenye hafla hiyo.
Taarifa ya Ikulu ilifafanua kuwa,
madawati mengine 60,000 yatatengenezwa kwenye awamu ya pili.
Rais Magufuli aliongeza kuwa,
ukigawa idadi ya siku 90 kwa vyombo viwili vya JKT na Magereza, maana yake kila
chombo kimetengeneza madawati 30,000.
Rais Magufuli alisema JKT ina kambi
nyingi na kutolea mfano za Oljoro, Makutupora, Mafinga, Mpwapwa, Mlale na
kwamba ukigawa kwa idadi ya kambi hizo kwa madawati 30,000 unapata wastani wa
madawati 30 kwa siku, ambayo yametengenezwa na kila kambi.
Kutokana na hali hiyo, amewataka
wakuu wa JKT na Magereza kuchukua jukumu hilo la utengenezaji madawati kama
vita, kwa kuwatumia wafungwa na nguvu kazi zilizopo katika vikosi kuharakisha
utengenezaji wa madawati.
Katika shughuli hiyo alikabidhi
madawati hayo kwa wabunge wa mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Lindi,
Mtwara, Ruvuma, Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe, Rukwa, Katavi, Unguja, Pemba na
Tanga.
Madawati hayo yalitengenezwa
kutokana na hundi ya Sh. bilioni nne iliyotolewa na Bunge na kukabidhiwa Rais
Magufuli Aprili 11, mwaka huu kama mpango wao wa kubana matumizi.
“Natoa wito kwa vyombo vya ulinzi,
JKT na Magereza japokuwa mmetengeneza madawati lakini mjipange katika hili,
haiingii akilini, nimekaa JKT mwaka mzima najua hamuwezi kutengeneza madawati
machache hivi,” alisema Magufuli.
“Niwaombe, chukueni hili kama
jukumu la haraka, tunahitaji madawati, ninahitaji madawati leo na Waziri Mwinyi
(Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Hussein Mwinyi) yupo hapa na kwa
bahati mbaya hajaenda JKT hajui shida tunazozipata kule, labda siku mumpeleke
siku akaone, sisi tunafahamu kule ni kazi tu,” alisema Rais
Magufuli.
Alisema JKT na Magereza wana nguvu
kazi kubwa wakiwamo wafungwa ambao hawahitaji fedha yoyote kufanya kazi kwani
ni wajibu wao, na kwamba kila mkoa kuna magereza hivyo askari waliopo katika
magereza hayo wakafanye kazi.
Alisema wafungwa waliofungwa katika
magereza wanapewa chakula kutoka katika bajeti kuu, hivyo wanapaswa kufanya
kazi.
Rais Magufuli alisema hata fedha
anazotarajia kuzipata kwa ajili ya utengenezaji wa madawati mengine kutoka
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na
PPF anasita kuvipatia vyombo hivyo vya ulinzi na usalama kwa kuogopa kuchukua
muda mrefu.
“Kama mmeshindwa mniruhusu niwa
‘involve’ wakuu wa mikoa, nina uhakika nikimwambia Makonda akiwahusisha vijana
wa vijiweni mwezi mmoja madawati yataisha. Sasa mnisaidie ndugu zangu makamanda
mkatengeneze madawati. Nimeona bora niongee hapa ili nisitoke na kiungulia, ila
nyie ndiyo mtoke na kiungulia,” alisema Magufuli
Rais Magufuli alisema anahitaji
madawati haraka ili kuondoa uhaba unaozikabili shule za sekondari na msingi wa
madawati 1,400,000.
Alisema hadi sasa zaidi ya madawati
1,000,000 sawa na asilimia 88 ya madawati yaliyohitajika kwa shule za msingi na
asilimia 95.8 kwa shule za sekondari yamepatikana.
Rais Magufuli alisema kwa sasa kwa
shule za msingi imebaki asilimia 11.2 kumaliza tatizo la madawati, huku kwa
shule za sekondari imebaki asilimia 4.2,
Alisema tangu atoe agizo kwa wakuu
wa wilaya na mikoa ya kutengeneza madawati, halmashauri 25 zimefikia malengo
kwa upande wa shule za msingi na halmashauri 46 kwa shule za sekondari.
Katika mgawanyo wa madawati hayo,
mkoa wa Dar es Salaam ulipata madawati 5,370, mikoa mingine na idadi yao katika
mabano ni Pwani (4,833), Morogoro (5,907), Lindi (4,295), Mtwara (5,370),
Ruvuma (4,833), Iringa (3,757), Njombe (3,222), Mbeya (3,759), Songwe (3,222),
Rukwa (2,285), Katavi (2,683) Unguja (3,200), Pemba (1,800) na Tanga (6,444).
Kadhalika, Rais Magufuli alisema
baada ya kuanza kutekeleza ahadi ya kuondoa ada kwa shule za msingi na
sekondari, idadi ya wanafunzi waliojiandikisha kuanza darasa la kwanza
imeongezeka kutoka wanafunzi 1,282,100 hadi kufikia wanafunzi 1,896,584 sawa na
ongezeko la asilimia 84.5 hali iliyosababisha upungufu wa madawati 1,400,000.

No comments:
Post a Comment