
Agizo la Jeshi la Polisi nchini la kusitisha kufanyika kwa mikutano ya hadhara ya kisiasa imeonekana kutoathiri ratiba za Mbunge wa Bariadi, John Chenge ambaye ameendelea na mikutano ya hadhara jimboni kwake.
Taarifa kutoka jimboni humo
zimeeleza kuwa Chenge amekuwa akifanya mikutano ya hadhara katika vijiji
mbalimbali na Alhamisi iliyopita alianza na eneo la Buchani, mkutano
uliomalizika salama bila kuwepo kizuizi chochote.
Katika mikutano hiyo, Mtemi Chenge
ameendelea kuwasisitiza wananchi wake kupuuza kauli za kisiasa zinazotolewa na
wapinzani wake bali waangalie namna anavyotekeleza ahadi alizozitoa kwenye
kampeni za uchaguzi mkuu.
Mikutano hiyo ya Chenge hutanguliwa
na matangazo yanayofanywa kwa kutumia magari yenye vipaza sauti katika eneo
husika.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu,
Onesmo Lyanga alipotafutwa kwa njia ya simu alisema kuwa yeye hahusiki kutoa
vibali vya mikutano na kwamba mhusika ni Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD). Hata
hivyo, OCD hakupatikana kwa wakati.
Hali hiyo imedaiwa kuzua
manung’uniko kwa vyama vya upinzani mkoani humo ambavyo vimeshindwa kufanya
mikutano ya hadhara kutokana na kuwepo kwa zuio la Mikutano hiyo nchi nzima.
Mwezi uliopita, Kamishna wa Jeshi
la Polisi, Operesheni ya Mafunzo, Nsato Msanzya alitangaza kupiga marufuku
kufanyika kwa mikutano ya kisiasa kwa sababu za kiusalama.
“Polisi kupitia vyanzo vyake
mbalimbali, imebaini kuwea mikutano hiyo ina lengo la kuwahamasisha wananchi
kutotii sheria za nchi,” alisema Kamishna Nsato.
Kufuatia agizo hilo, Jeshi la
Polisi lilizuia kufanyika kwa mikutano iliyokuwa imepangwa na Chadema na
ACT-Wazalendo kwa nyakati tofauti.

No comments:
Post a Comment