Waziri mkuu mpya wa
Uingereza, Theresa May amemteua Boris Johnson kuwa waziri wa Mambo ya Nje na
Philip Hammond kuwa Waziri wa Fedha wa nchi hiyo.
Aidha
Amber Rudd ameteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Michael Fallon ameteuliwa
kuwa Waziri wa Ulinzi.
Waziri Mkuu huyo mpya wa Uingereza amesema kuwa serikali yake
haitanaswa na mtego wa kuwasikiliza watu walio wachache na kusahau wananchi wa
kawaida. Theresa May anakuwa waziri mkuu wa 13 kuwahi kuiongoza Uingereza
katika enzi ya Malkia Elizabeth wa pili.
Hapo jana waziri mkuu aliyetangaza kujiuzulu hivi karibuni,
David Cameron alihutubia kwa mara ya mwisho Bunge la Uingereza na kujibu
maswali ya wabunge wa Bunge hilo na baadaye aliwasilisha barua yake ya
kujiuzulu kwa Malkia Elizabeth wa Pili kwenye Kasri lake lililopo huko
Buckingham.
Malkia amemtaka Bi May kuunda serikali ikiwa ni historia ya
pekee kwa Uingereza kupata kiongozi wa pili mwanamke baada ya Margaret
Thatcher.
Viongozi wa Umoja wa Ulaya (EU) wameitaka serikali ya Uingereza
kuharakisha mchakato wa kujitoa rasmi katika umoja huo, lakini May amedokeza
kuwa hatauharakisha mpango huo mashuhuri kwa jina la Brexit.
Changamoto kubwa inayomkabili Waziri Mkuu huyo mpya wa Uingereza
ni pamoja na kuizuia Scotland inayounga mkono Umoja wa Ulaya dhidi ya kuitisha
kura ya uhuru wake ili kubakia katika EU na kuimarisha mahusiano mapya ya
kibiashara na kidiplomasia ili kujiandaa kwa hali ya baadaye ya baada ya
kujiondoa katika umoja huo.

No comments:
Post a Comment