
WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward
Lowassa amekuwa miongoni mwa mamia ya waombolezaji walioshiriki maziko ya
mbunge wa zamani, Beatrice Shelukindo (58) yaliyofanyika nyumbani kwa wazazi
wake katika kata ya Olorien Jijini Arusha jana.
Viongozi wengine waliohudhuria
maziko hayo yaliyotanguliwa na ibada ni pamoja na Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, Jaji Mkuu mstaafu, Agustino
Ramadhani, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Felix Ntibenda.
Pia maziko hayo yalihudhuriwa na
wabunge na viongozi mbalimbali wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutoka Mkoa wa
Tanga na Arusha, Meya wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Kalisti Lazaro na
viongozi wengine wa vyama vya siasa na serikali.
Ibada ilifanyika katika Kanisa Kuu
la Anglikana, Dayosisi ya Mount Kilimanjaro ambako Askofu mstaafu, Simon
Makundi, alisema Beatrice hakuwa fisadi na alitoa mchango mkubwa kwa familia,
dini, taifa na Afrika Mashariki.
“Jiulize wewe una mchango gani hata
katika familia yako, dini yako, taifa hili na hata kwa Afrika Mashariki?” Alihoji
Makundi.
Aliwataka mamia ya waombolezaji
wakipewa nafasi, heshima na vyeo serikalini au katika kampuni yo yote kuitunza
heshima hiyo kwa kufanya kazi kwa uadilifu na kuwa na hofu ya Mungu.
Beatrice aliyezaliwa mwaka 1958
amefariki akiwa na umri wa miaka 58, jambo ambalo askofu mstaafu alisema hiyo
ni neema ya Mungu.
Alisisitiza kuwa Beatrice alifanya
kazi za utumishi serikalini na ubunge kwa uadilifu mkubwa na kupata heshima na
serikali, dini na jamii na ndiyo maana aliweza kuhitimisha heshima hiyo hadi
mwisho. Askofu Makundi alisema alipata bahati ya kuzungumza naye kabla ya
mauti.




No comments:
Post a Comment