
MBUNGE wa Bunge la Afrika Mashariki
(EALA) kutoka nchini Burundi, Hafsa Mossi, ameuawa na watu wasiojulikana kwa
kupigwa risasi katika mji mkuu wa Bujumbura.
Mossi aliyewahi kuwa Waziri wa
Masuala ya Afrika Mashariki katika serikali ya nchi hiyo, aliuawa jana katika
barabara ya Gihosha eneo la Nyankoni.
Taarifa zilizothibitishwa na
Msemaji wa Polisi wa nchi hiyo, Pierre Nkurikiye zilisema kuwa mauaji hayo
yalifanyika saa 4:00 asubuhi. Nkurikiye alisema mbunge huyo alipigwa risasi
kifuani kwenye moyo na kukimbizwa katika Hospitali ya Jeshi ya Kamenge ambako
baadaye alipoteza maisha.
EALA ni chombo cha Jumuiya ya
Afrika Mashariki (EAC) ambacho wanachama wake ni Kenya, Uganda, Tanzania,
Rwanda, Burundi na Sudan Kusini, ukiwa ni umoja wa kikanda wenye ushirikiano wa
kibiashara huku ukikusudia kuwa na sarafu moja na shirikisho moja la kisiasa.
Mkazi wa eneo alikouawa Mbunge
huyo, Achel Majabuka alisema kuwa alisikia mlio wa risasi na baadaye kuona watu
wawili wakiondoka katika gari baada ya kuwatishia kwa silaha wakazi wa eneo
hilo.
Kwa upande wake, Bunge la Afrika
Mashariki katika taarifa yake iliyotolewa Kampala nchini Uganda, ilisema kuwa
Mossi ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Wabunge wa Burundi katika EALA, alipigwa
risasi katika eneo la Mulanga Mashariki mwa Bujumbura.
Alimkariri msemaji huyo wa Polisi
akieleza kuwa Mossi aliuawa karibu na nyumbani kwake, huku Mbunge mwingine wa
Burundi katika EALA, Emerence Bucumi akithibitisha kifo hicho.
Spika wa Bunge la Afrika Mashariki,
Daniel Kidega alilaani mauaji hayo na kumuelezea Mossi kuwa ni mchapakazi
aliyekuwa amejikita kusimamia na kutetea utengamano wa ukanda huo.
Spika huyo ambaye yuko Uganda kwa
ziara ya kikazi, ameishauri Serikali ya Burundi kuwatia nguvuni mara moja
wauaji wa Mossi ambaye pia aliwahi kuwa Mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la
Uingereza (BBC).
“Ninatoa salamu za rambirambi kwa
serikali, familia, marafiki na wananchi wa Burundi. Ninawaomba wawe watulivu
katika wakati huu mgumu na ninaamini mamlaka husika zitafanya kazi kwa haraka
kuhakikisha waliohusika na tukio hilo la kinyama wanatiwa nguvuni mara moja,” alisema
Spika Kidega.
Kwa upande wake, Rais wa Burundi,
Pierre Nkurunziza alikielezea kifo cha mwanasiasa huyo kuwa ni cha kudharauliwa
kwa serikali yake. Naye Katibu Mkuu wa EAC, Balozi Liberat Mfumukeko, alisema
amesikitishwa na kifo hicho cha Mbunge huyo aliyeeleza alikuwa rafiki na dada
na kuwa jumuiya imepoteza mwakilishi aliyekuwa akifanya kazi bila kuchoka.
Mwaka jana, Mossi alitembelea
wakimbizi wa Burundi nchini Rwanda na kulia, ameuawa wakati mazungumzo kuhusu
mgogoro wa Burundi yakiwa yanaendelea kufanyika jijini Arusha.
Alikuwa na Shahada ya Uandishi wa
Habari na aliwahi kufanya kazi katika BBC na alikuwa Waziri wa Burundi wa
Masuala ya Afrika Mashariki hadi Juni 2012 alipochaguliwa kuwa Mbunge wa EALA.
Pia, aliwahi Waziri wa Mawasiliano,
Habari, Mahusiano na Bunge na Msemaji wa Serikali ya Burundi kuanzia mwaka 2005
hadi 2007.
Burundi, taifa katika Afrika
Mashariki imekumbwa na ghasia na vifo kwa zaidi ya mwaka sasa.
Mgogoro huo wenye kuendana na
umwagaji damu, umesababisha watu 1,500 kuuawa, huku ukiwahusisha wafuasi wa
Rais Nkurunziza na wale wanaopinga ushindi wake wa uchaguzi wa Julai, 2015 kwa
mara ya tatu, wakidai kuwa ulikiuka Katiba ya nchi hiyo.

No comments:
Post a Comment