
WAZIRI wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi,
Dk Charles Tizeba amewasimamisha kazi wakurugenzi watano wa idara tofauti
katika wizara hiyo kutokana na kuonesha udhaifu mbalimbali katika utendaji wao
na wengine kusababisha hasara katika usalama wa chakula.
Waliosimamishwa kazi ni Kaimu
Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Chakula nchini, Ombaeli Lemweli kutokana na
kutoa vibali vya ununuzi wa mazao na kuuzwa nje ya nchi ilhali tathmini ikiwa
haijafanyika. Nafasi yake kuchukuliwa na Elimpaa Kiranga aliyekuwa Mkurugenzi
wa Bodi ya Mazao Mchanganyiko.
Aidha, ameagiza kusimamishwa kazi
kwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Charles
Walwa na nafasi yake kushikwa na Deusdedit Mpazi aliyekuwa Meneja wa NFRA kanda
ya Dodoma, kutokana na kuharibu ghala la chakula na kusababisha hasara.
Viongozi wengine wa NFRA
waliosimamishwa ni Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Huduma, Anna Ngoo, Mkurugenzi wa
Masoko, Mikalu Mapunda na Meneja wa NFRA, Songea Jeremia Mtafya ambao
wametakiwa kupisha na uchunguzi kufanyika mara moja dhidi yao.
Kadhalika, Dk Tizeba amemsimamisha
kazi aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bahari Kuu, Rashid Hoza na nafasi
yake kushikwa na Hosea Mbilinyi aliyekuwa Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi, lengo
likiwa ni kuimarisha ulinzi wa Bahari Kuu.
Mbali na nafasi hizo, pia Mkuu wa
Kituo cha Utafiti cha Uyole mkoani Mbeya, Dk Zakaria Maly amevuliwa madaraka na
kuhamishiwa katika Kituo cha Utafiti Seliani mkoani Arusha kuendelea na utafiti
na badala yake nafasi yake itachukuliwa na Arnold Msongi anayetoka Kituo cha
Utafiti Ilonga, Kilosa mkoani Morogoro.
Dk Tizeba alitoa maamuzi hayo jana
Dar es Salaam wakati akizungumzia masuala mbalimbali, ikiwa ni mwezi mmoja
baada yakuteuliwa na Rais John Magufuli kushika wadhifa huo katika mabadiliko
madogo ya Baraza la Mawaziri yaliyompeleka aliyekuwa waziri wa wizara hiyo,
Mwigulu Nchemba kuongoza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Waziri Tizeba alisema wakati ambapo
tathmini ya chakula nchini ikiwa haijakamilika, Kurugenzi ya Usalama wa Chakula
imekuwa ikitoa vibali vya chakula kusafirishwa nje ya nchi, huku ikiwa
haijulikani kama chakula kilicho kinatosha au hakitoshi na ili ziada ilindwe.
“Mbali ya kwamba hali ya chakula
nchini ni nzuri lakini kumekuwepo na wimbi la wafanyabiashara wa ndani na nje
ya nchi wakipewa vibali na kununua mazao ndani ya nchi na kuyauza nje ilhali
tathmini ikiwa haijakamilika,” alisema Tizeba.
Alitoa wiki mbili kuanzia sasa
ukaguzi wa chakula nchini uwe umefanyika ili kupatikana kwa tathmini halisi
katika kipindi cha mwaka 2015/2016 kwani ununuzi wa mazao hayo umeonekana
mkubwa na hali hiyo isipodhibitiwa hali itakuwa mbaya zaidi.
Alisema vibali hivyo vimekuwa
vikitolewa kinyume cha utaratibu kwa kuwa tathimini ilitakiwa kufanyika kwanza,
hivyo Katibu Mkuu amsimamishe kazi mkurugenzi huyo na uchunguzi ufanyike dhidi
yake pamoja na vibali ambavyo vimekuwa vikitolewa tangu mwaka jana kwani havina
harufu nzuri.
“Hata hivi karibuni nimepata
taarifa kuna mfanyabiashara kapewa kibali cha kusafirisha tani laki tatu
kupeleka nchini Malawi, mfanye uchunguzi wa vibali vyote alivyovitoa,” alisema
Tizeba.
Kuhusu NFRA, Dk Tizeba alisema
umekuwepo udhaifu mkubwa katika ghala la Songea, Dodoma na Sumbawanga ambako
mazao yameharibika na kusababisha hasara huku uongozi wa wakala licha ya
kuombwa vibali vya kununuliwa kwa mazao hayo kama chakula cha mifugo
havikutolewa.
Akizungumzia uvuvi bahari kuu,
ameiagiza Kurugenzi wa Uvuvi kubadilisha masharti ya leseni ya uvuvi katika
bahari kuu ili kuangalia uwezekano wa kufanya ubia na wavuvi hao ili Watanzania
nao waweze kunufaika na mavuno ya mazao hayo.
Alisema kwa wale ambao wana leseni
hazitofanyiwa mabadiliko lakini kwa zile mpya na sheria haizuii kufanya hivyo.
Alisema hivi sasa zipo meli 105
zote zikitoka nje ya nchi zikiwa zinaendelea na uvuvi na kuchota chochote na
kuondoka, huku mamlaka ya bahari wakiwa wanayajua hayo, wakidai kuwa Tanzania
haina mahali pa kushushia.
Alisema kuanzia sasa meli zote
ziambiwe mazao yote watakayovuna ambayo ni tofauti na leseni zao zinavyotaka
yaletwe Dar es Salaam, yagawiwe kama itakavyohitajika kwani Tanzania imeendelea
kuwa shamba la bibi kutokana na kukosa uwezo wa kuvua katika bahari kuu.

No comments:
Post a Comment