
Jeshi la Polisi jana liliwahoji
Mhariri Mtendaji wa Mwananchi, Frank Sanga na mwandishi wa habari, Elias Msuya
kuhusu makala iliyochapishwa juzi kuhusu utendaji wa jeshi hilo.
Baada ya mahojiano yaliyofanyika
kwa muda tofauti, waliachiwa kwa dhamana na kutakiwa kuripoti kituoni hapo leo
asubuhi.
Msuya ndiye aliyeanza kuhojiwa
baada ya juzi jioni kupigiwa simu na maofisa wa polisi akitakiwa kufika Kituo
Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam kuhojiwa kutokana na makala yake ya
uchambuzi yenye kichwa cha habari “Polisi na hofu ya watawala kuondoka
madarakani.”
Makala hayo yalichapishwa katika
gazeti hilo toleo la Julai 13 na mwandishi huyo alieleza mambo mbalimbali
yanayohusu utendaji wa jumla wa jeshi hilo kwa wananchi.
Baada ya kutoa maelezo kwa saa
mbili, maofisa hao walimpigia simu Sanga na kumtaka afike kituoni hapo kwa
ajili ya kuhojiwa kuhusu makala hiyo.
“Wamenihoji maswali mbalimbali
kuhusiana na makala niliyoandika. Nimewajibu kulingana na jinsi walivyokuwa wakiniuliza,” alisema
Msuya.
Msuya alifika katika kituo hicho
saa moja asubuhi na kukaa kwa saa mbili kabla ya kuanza kuhojiwa na kisha Sanga
ambaye alifika kituoni hapo mchana na kuhojiwa kwa dakika 90.
Akizungumzia suala hilo, Mhariri
Mtendaji Mkuu wa Mwananchi Communications Ltd (MCL), Bakari Machumu alisema
baada ya wito huo wa polisi, kampuni imetoa ushirikiano wa kutosha kwa
kuwaruhusu Sanga na Msuya kwenda kutoa maelezo polisi.
Alisema ni vyema masuala yanayohusu
habari ambazo zinatakiwa kutolewa ufafanuzi yakaihusisha Wizara ya Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo na Baraza la Habari Tanzania (MCT).
“Nadhani jambo kama hili
kuchukuliwa moja kwa moja na polisi ni kama kuingilia uhuru wa habari. Vipo
vyombo vinavyoweza kutoa ufafanuzi wa habari iliyoripotiwa na vyombo vya
habari,” alisema Machumu.
Baada ya mahojiano hayo, Sanga na
Msuya waliachiwa kwa kila mmoja kudhaminiwa na mtu mmoja.

No comments:
Post a Comment