
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA)
imetoa mashine 130 za kielektroniki za kutoa risiti (EFDs) kwa Makatibu Wakuu
25 wa wizara zote nchini kwa ajili ya taasisi na mamlaka zao, zenye wajibu wa
kukusanya mapato ya serikali ili kuhakikisha wanaokoa mapato ya serikali
yanayopotea.
Akizungumza jana Dar es Salaam
wakati wa kukabidhi mashine hizo, Kamishna Mkuu wa TRA, Alphayo Kidata alisema
kila wizara itapewa mashine tano ili kuboresha ukusanyaji wa mapato.
“Kila Katibu Mkuu tunamkabidhi
mashine tano za EFDs zitakazosaidia kuhakikisha serikali inapata mapato yake na
hivyo kuokoa mapato ya serikali ambayo yanapotea,” alisema na
kuongeza:
“Tunatarajia mashine hizi
zitatumika mahususi kutolea risiti, hivyo watumishi wote wa serikali ambao
wanafanya marejesho ya matumizi mbalimbali wanatakiwa kuambatanisha risiti za
mashine za EFDs”.
Aidha alisema TRA inaendelea kudhibiti
wafanyabiashara wanaokwepa kutumia mashine za kielektroniki za kodi kwa
kuwakamata na kuwatoza faini au kuwafikisha mahakamani kwa hatua zaidi za
kisheria.
“Lengo letu ni kuhakikisha
tunafikia na kuvuka lengo la kukusanya Sh trilioni 15.5 kwa mwaka wa fedha
2016/2017 ambao tayari tumeuanza,”alisema.

No comments:
Post a Comment