
Katika siku za hivi karibuni
kumekuwa na Uvumi katika Mitandao ya Kijamii kuwa Serikali imeamua kushusha
Mishahara ya Madaktari kwa asilimia 30% ili kuendana na dhana ya Hapa kazi tu
na kuwa Serikali imekusudia kufuta malipo ya Posho za Wataalamu wa
Afya walio katika Mafunzo kwa Vitendo .Ufafanuzi kwa Umma wa Watanzania na
Watumishi wa Sekta ya Afya ni kuwa taarifa hizo siyo za kweli.
Taarifa aliyoitoa Katibu Mkuu
(Afya) alipokuwa anaongea na Watumishi wa Hospitali ya Bugando
ililenga kutoa ufafanuzi kwa Watumishi wa Hospitali hiyo kuhusu kufutwa kwa
kibali cha Msajili wa Hazina kilichowawezesha watumishi wa Hospitali hiyo
kulipwa Mishahara ya Taasisi zilizo chini ya Msajili wa Hazina tangu mwaka
2012.
Uamuzi huo wa Msajili wa Hazina
unatokana na ukweli kwamba Hospitali ya Bugando siyo Shirika la Umma na hivyo
wanastahili kulipwa mishahara sawa na watumishi wengine wa Serikali Kuu kwa
kuzingatia makubaliano yaliyopo kati ya Serikali na Baraza la Maaskofu
Tanzania (TEC) ambao ndio wamiliki wa Hospitali ya Bugando.
Aidha, ieleweke kuwa mishahara ya
Watumishi wa Sekta ya Afya haizingatii ngazi ya Vituo vya kutolea huduma kama
vile Zahanati, Kituo cha Afya, Hospitali, au Hospitali za Rufaa bali huzingatia
uzito wa kazi na majukumu ya kada husika. Hivyo, mshahara wa Daktari wa
Hospitali ya Wilaya ni sawa na ule wa Hospitali ya Rufaa ngazi ya Mkoa na
Hospitali ya Rufaa ya Kanda.
Kutokana na maelezo haya, uamuzi
huo wa Msajili wa Hazina utaihusu Hospitali ya Bugando pekee na siyo Hospitali
zote za Kanda kwa kuwa dosari hiyo haikutokea katika Hospitali nyingine za
Kanda.
Kuhusu ajira mpya kwa mwaka
2015/2016 ufafanuzi ulitolewa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kwamba hakutakuwa na ajira mpya hadi hapo Zoezi la Uhakiki wa Watumishi
Serikalini litakapokamilika. Hivyo, vibali vya ajira vilivyokuwa
vimetolewa vimefutwa hadi hapo itakapotamkwa vinginevyo.
Kadhalika, kumekuwa na Uvumi kuwa
Serikali inakusudia kufuta posho ya ‘Interns' kuanzia mwaka huu wa fedha.
Taarifa hii pia siyo sahihi kwa kuwa hakuna chombo chochote cha Serikali
ambacho kimetoa maamuzi hayo.
Wizara inasisitiza kuwa maamuzi ya
Serikali hutolewa na Mamlaka husika kwa nyaraka. Hivyo, watumishi wa
Sekta ya Afya na wananchi kwa ujumla wanaaswa kuzingatia taarifa zinazotolewa
na Mamlaka za Serikali kuhusu Masuala yanayowahusu ambayo mara nyingi hutolewa
kwa nyaraka badala ya Mitandao ya kijamii,
Imetolewa na;
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
– Afya
14 Julai, 2016

No comments:
Post a Comment