
UMOJA wa Vijana wa Chama cha
Wananchi (JUVICUF), umeapa kutotoa ushirikiano wa kikazi kwa viongozi wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM) walioteuliwa na Rais John Magufuli ambao wanatoa
matamko yasiyo na tija kwa wananchi.
Mkuu wa Idara ya Habari na Uenezi
wa JUVICUF, Dahlia Majid alisema katika mkutano na waandishi wa habari Dar es
Salaam jana kuwa uteuzi wa makada wa CCM katika nafasi za wakuu wa wilaya
pamoja na wakurugenzi utavuruga nchi hususani katika kipindi cha uchaguzi.
Akisoma tamko hilo kwa niaba ya
Mwenyekiti wa JUVICUF Taifa, Hamidu Bobali, Dahlia alisema viongozi wa awamu ya
tano wanakurupuka na kutoa matamko yasiyo na tija yanayobaka mamlaka ya Jeshi
la Polisi.
“Haiwezekani viongozi wa awamu ya
tano wanakurupuka tu wanatoa matamko yasiyo na tija kila siku tena mengine
yanabaka mamlaka hata ya mahakama na wanajifanya wao ndio polisi, wao ndio
mahakama na wao ndio magereza, tutawaagiza viongozi wetu katika halmashauri
zinazoongozwa na CUF kukataa kauli na matamko ya namna hiyo.
“JUVICUF tunakitaka Chama cha CUF
kuwaagiza viongozi wake katika halmashauri tunazoziongoza kwamba waache mara
moja kutekeleza maagizo yasiyo na tija kutoka kwa viongozi waliolewa madaraka.
“Tunawasihi vijana waendelee na
shughuli zao za kujiletea maendeleo bila kujali matamko yanayotolewa na
viongozi waliolewa madaraka na kujifanya miungu watu,” alisema.
Dahlia alitolea mfano wa agizo
lililotolewa hivi karibuni na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda la
kuwakamata wananchi wasiokuwa na kazi maalumu ambapo alisema hayo ni miongoni
mwa maagizo ya ovyo na hayapaswi kutekelezwa.
Kiongozi huyo wa vijana alisema
agizo hilo ni kinyume cha sheria huku akitahadharisha kuwa utekelezaji wake
utahusisha askari kupiga watu, visa na vijana kubambikiwa kesi zisizokuwa na
sababu.
“Ni ajabu sana na hii haipo kote
duniani kibali cha kuwakaguwa wananchi majumbani kutolewa na viongozi wa
kisiasa, mahakama zina kazi gani? serikali imefanya maisha kuwa magumu na ajira
kuwa ngumu kupatikana halafu wao wanaibuka na sera ya kukamata watu wasio na
ajira,” alisema Dahlia.

No comments:
Post a Comment