
MPIGACHAPA Mkuu wa Serikali,
Cassian Chibogoyo amekiri kuwepo kwa nyaraka bandia za serikali katika sekta
mbalimbali, nyingi zikiwa za ukusanyaji wa mapato ya serikali, vyeti vya
kitaaluma, ndoa na nyinginezo.
Kutokana na hali hiyo, amewaasa
wananchi wanaofanya shughuli hizo za kutengeneza nyaraka hizo bandia ambazo ni
hatari kwa usalama wa nchi, kuacha kwani wanaendesha oparesheni ya kudumu
itakayowabaini na kuchukuliwa hatua kali, ikiwemo kifungo cha miaka 20 jela.
Hivyo amewataka watendaji na
wasimamizi katika idara mbalimbali kufanya uhakiki upya wa nyaraka za serikali,
kwani zimezagaa sehemu mbalimbali nchini hususan katika Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA), vyuoni na katika maeneo ya kazi.
Akizungumza Dar es Salaam jana,
Mpigachapa Mkuu Chibogoyo alisema nyaraka hizo bandia ni pamoja na stakabadhi
za malipo, vibali mbalimbali, hati za makontena, leseni za magari pamoja na
bima.
Alisema katika oparesheni
iliyofanyika mwaka jana ya ‘Okoa Pato la Taifa‘ katika kutafuta nyaraka bandia
za serikali, walibaini kuwepo kwa nyaraka za vyeti vya ukaazi au kuzaliwa
vinavyomilikiwa na raia wa kigeni, stakabadhi za mapato, leseni za biashara,
vyeti bandia vya kitaaluma na vinginevyo.
Alisema nyaraka hizo walizikuta katika
vituo vyao vya mauzo na wengine kwenye nyumba zao za kutengenezea uhalifu huo
na kubaini kuwa uhalifu huo ni zaidi ya ujambazi kutokana na madhara yake kwa
nchi.
Alisema katika oparesheni hiyo
walibaini kiwanda cha kutengeneza bidhaa hizo maeneo ya Buguruni katika
Manispaa ya llala, Dar es Salaam pamoja na vyeti feki vya Chuo Kikuu cha
Kampala (KIU), vitambulisho vya ukaazi ambako kuna raia wa kigeni amepewa cha
ukazi akiishi Kariakoo, risiti za usalama barabarani pamoja na shahada za ndoa
za Kanisa Katoliki la Mtakatifu Maria Magomeni jijini Dar es Salaam.
Alisema pia walikamata boksi tatu
za stika za bima zinazowekwa kwenye magari zikiwa tayari kusafirishwa kwenda
mkoani Tanga zikiwa zimewekwa kwenye jokofu bovu lililochakaa karibu na mama
ntilie katika maeneo ya Salamander.
“Wananchi wasio waaminifu wanaotaka
kupoteza maisha ya wananchi wema na usalama wa nchi ikiwemo kurudisha nyuma
maendeleo na uchumi wa nchi, nawapa salamu zangu kuwa mimi na timu yangu
tumejipanga kutokomeza vitendo hivyo na tutapigania nchi,” alisema
Chibogoyo.
Alieleza kuwa makatazo ya udhibiti
wa nyaraka yapo katika Sheria ya Makosa ya Jinai, Sheria ya Ngao ya Taifa,
Sheria ya Ushahidi na Sheria ya Usalama wa Taifa, hivyo ukikamatwa na katatasi
inayokusudia kutumika kwa udanganyifu, adhabu ni kufungwa miaka saba.
Aidha, alifafanua kuwa Sheria ya
Usalama wa Taifa ya mwaka 1970 inakataza kuwa na nyaraka, mihuri, karatasi
maalumu na kumiliki taarifa za serikali isivyo halali na sheria inasema kuwa ni
mhalifu na adhabu yake ni miaka 20 jela.
Chibogoyo aliwataka wananchi wema
kutoa taarifa pale wanapowabaini watu hao wanaotengeneza nyaraka bandia za
serikali pale wanapohitaji nyaraka hizo kwa haraka na ofisi yake itampatia
nyaraka halali kwa haraka.
Akizungumzia nyaraka hizo bandia za
serikali, Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro
alisema hali ya nyaraka hizo inatisha kwani ni kubwa kwani nyaraka hizo zote
muhimu zipo na zinatumika katika maeneo mbalimbali.
Kamanda Sirro alisema kuna watu wamenufaika
kwa nyaraka hizo kama vyeti kutumika kupata ajira hivyo watafuatilia na
watawachukulia hata za kisheria wanufaika wote wa nyaraka hizo bandia.
Alisema katika oparesheni
waliyoshirikiana na Mpigachapa Mkuu wa Serikali walikamata watu watatu ambao
inaonekaan ndiyo mabosi au wakurugenzi wa kutengeneza nyaraka hizo huku wakiwa
na mawakala wao katika mikoa mbalimbali kama Mwanza na kwingineko.
Alisema wataendelea kufanya
oparesheni ili kuhakikisha suala hilo linakoma kwa kuwakamata wahusika wote.

No comments:
Post a Comment