
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu,
Dar es Salaam imetupilia mbali maombi ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu
Lissu (Chadema) ya kufutiwa mashitaka ya uchochezi yanayomkabili na wenzake
watatu.
Hakimu Mkazi Mkuu, Emillius Mchauru
alitoa uamuzi huo jana baada ya kukubali pingamizi lililowasilishwa na upande
wa Jamhuri waliodai mashitaka hayo yasifutwe kwa kuwa hati ya mashitaka haina
makosa.
Mbali ya Lissu, washitakiwa wengine
katika kesi hiyo ni mwandishi wa gazeti la Mawio, Jabir Idrissa, Mhariri wa
gazeti hilo, Simon Mkina na Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob.
Hata hivyo, uamuzi huo ulitolewa jana bila Lissu kufika mahakamani hapo kwa kuwa
anaumwa.
Akiieleza mahakama, Wakili wa
utetezi, Peter Kibatala alidai Lissu ameshindwa kufika mahakamani kwa kuwa
anaumwa, lakini wadhamini wake akiwemo Ibrahim Ahmed wamefika mahakamani na
kueleza kuwa Lissu anaumwa malaria. Aidha, ilielezwa kuwa mshtakiwa Idrissa
anaumwa na yupo Zanzibar kwa ajili ya matibabu.
Katika maombi yao, washitakiwa
kupitia kwa Wakili Kibatala waliiomba mahakama ifute mashitaka hayo kwa kuwa
hati ya mashitaka imekosewa kwa kutokueleza makosa hayo wametenda wapi na pia
mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza masuala yanayohusu Zanzibar.
Akisoma uamuzi, Hakimu Simba
alisema baada ya mahakama kupitia hoja za pande zote mbili katika kesi hiyo
imejiridhisha kuwa hati ya mashitaka haina makosa.
Aidha, alisema mahakama hiyo ina
mamlaka ya kusikiliza shauri hilo kwa kuwa makosa yaliyofanyika yanahusu
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hivi karibuni, mahakama ilifuta
mashitaka mawili ya uchochezi kati ya matano yanayowakabili washitakiwa hao,
baada ya upande wa jamhuri kuyaondoa katika hati kwa kuwa hayana kibali cha
Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).
Katika mashitaka yao inadaiwa
Januari 12 hadi 14, 2016, Dar es Salaam washitakiwa walichapisha taarifa ya
uchochezi yenye kichwa cha habari ‘ Machafuko yaja Zanzibar’.
Pia inadaiwa Januari 14, 2016 Dar
es Salaam walichapisha habari hizo ili kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar.
Inaendelea kudaiwa siku hiyo hiyo, Lissu na wenzake bila ya kuwa na mamlaka
yoyote yale waliwatisha na kuwatia hofu wananchi wa Zanzibar ili wasikubali
kuingia kwenye marudio ya Uchaguzi Mkuu.

No comments:
Post a Comment