
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe.Dk John Pombe Magufuli amewaagiza makatibu wakuu kuhakikisha
vyombo vyote vinavyokusanya mapato serikalini vinatumia mashine za
kielekrtoniki (EFD).
Rais Magufuli ameyasema hayo wakati
akizungumza na wakurugenzi wateule wa Halmashauri,Wilaya,Majiji na Manispaa
Ikulu jijini Dar es Salaam wakati wa kiapo cha ahadi ya uadilifu kwa viongozi
hao wa umma.
“Vyombo vya Serikali lazima vianze
kutumia mashine za EFD,haiwezekani wafanyabiashara wawe na mashine za EFD
alafu maafisa wa serikali hawana,kama tumeamua kwenda kwa elektroniki lazima
twende hivyo”Alisema Rais Magufuli.
Aidha amewataka wakurugenzi
wote kuchukua mashine hizi na kwenda nazo katika maeneo yao ya kazi ili
ziwasaidie katika ukusanyaji wa mapato ya serikali katika halmshauri zao.
Pia amewaagiza wakurugenzi hao
kukusanya kodi na kutatua kero za wananchi wa chini zisizokuwa na lazima na
kuongezea kuwa kama watakuta watendaji wa chini yao wasioendana na kasi
ya awamu ya tano basi watumie madaraka yao kuwaweka sawa.
Rais magufuli pia amewaagiza
wakurugenzi hao kusimamia ilani ya uchaguzi ya chama cha mapinduzi kwakuwa
waliahidi kutatua kero za wananchi na wahakikishe wanazitatua ili wananchi
waishi vizuri kwa amani ndani ya nchi yao na kuongezea kuwa viongozi wa juu
wana imani kubwa sana nao ndio maana hata wakachaguliwa kutoka katika
watanzania hawa milioni 50.
Aidha Rais magufuli amewataka
wakurugenzi hao kusimamia kuanzishwa kwa viwanda vidogo vidogo katika maeneo
yao ili kukamilisha azma ya serikali ya awamu ya tano ya kuwa na viwanda.
Mbali na hayo pia amewataka
wakurugenzi hao kubadilika kifikra na kuachana na kuongoza kwa historia kwani
wananchi wa sasa wamebadilika na hivyo wafanye kazi kwa bidii ili kuwatimizia
wananchi yale wanayotaka na hivyo nchi itasonga mbele.

No comments:
Post a Comment