MAMLAKA ya Udhibiti ya Huduma za
Nishati na Maji (EWURA) imesema kuna akiba ya kutosha ya mafuta ya aina
mbalimbali yanayoweza kutumika kati siku 13 hadi 39 nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Felix
Ngamlagosi, alisema hayo jijini Dar es Salaam jana katika mkutano na wadau wa
sekta ya mafuta nchini wa kupokea maoni juu ya mfumo wa uingizaji wa mafuta
nchini.
Tamko la EWURA limekuja kukiwa na
tatizo la uhaba wa mafuta ya petrol, dizeli na mafuta ya taa katika baadhi ya
mikoa hali iliyosababisha wananchi wa mikoa iliyokumbwa na tatizo hilo kupata
adha.
Ngalamgosi alisema akiba ya mafuta
ya ndege iliyopo inatosha kutumika kwa siku 30 kwa nchini nzima, petroli ni
zaidi ya siku 12, dizeli ni zaidi ya siku 15, mafuta ya taa ni zaidi ya siku
16, mafuta ya viwandani ni zaidi ya siku 39 na mafuta ya migodini zaidi ya siku
13.
Alisema sababu ya kutokea uhaba wa
mafuta unaoonekana sasa ni kuwepo kwa sikukuu zilizofululiza na kusababisha
magari ya kubeba mafuta kushindwa kusafirisha mafuta, na ama kufika kwa wakati
katika mikoa hiyo iliyokubwa na kadhia hiyo.
Jumatano na Alhamisi zilizopita
palikuwa na siku kuu za Eid el Fitri.
“Niwaombe Watanzania wawe na subira
kwani mafuta yapo yakutosha, hivyo nawaomba wasinunue mafuta kwa kupaniki kwani
magari ya kusafirisha mafuta yameanza kusambaza katika mikoa hiyo na hali
itatulia kuanzia sasa,” alisema.
Alisema magari ya mafuta
yameshapeleka shehena katika mikoa ya Mtwara, Ruvuma, Songea na Mbinga ambako
hali ya upatikanaji wa mafuta imeanza kutulia.
Mafuta ya taa
Ngalamgosi alisema uhaba wa mafuta
ya taa ulitokana na meli iliyokuwa ikishusha mafuta ya ndege na petroli
kuyachaganya wakati wa kuyasukuma.
Alisema kuwa kutokana na
mchanganyiko huo ni wazi kuwa mafuta ya ndege ambayo ndio hutumika kama mafuta
ya taa, hayaweza kutumika kwa matumizi ya kawaida.
“Mafuta ya ndege ndio hayo hayo
yanatumika kama mafuta ya taa hivyo kutokana na kuchanganyika huko ilipaswa
kusafisha matanki yote na mabomba ili kuweka mafuta mapya,” alisema.
Alisema zoezi la kuyasafisha
matanki matano lilifanyika kwa wiki tatu mfululizo na kukamilika Julai 2, kabla
ya kuanza kupokea mafuta na kuyasambaza Julai 3 mwaka huu katika mikoa ambayo
kulitokea uhaba.
Kampuni za ndani
Ngalamgosi alisema EWURA
imependekeza kubadilishwa kwa mfumo wa uingizwaji wa mafuta nchini kutoka
nchini za nje kwa kuanzishwa mfumo mpya wa kutoa fursa kwa kampuni za ndani
kuingiza mafuta nchini.
Ngalamgosi alisema kuwa amekutana
na wadau wa sekta ya mafuta ili kupokea maoni ni namna gani wanaweza kuboresha
ushindani na wamependekeza kuwa kila meli inayokuja lazima iwe na zabuni yake.
Alisema Tanzania inaingiza meli
sita za mafuta kwa mwezi, hivyo EWURA imeona kuwa inapasa kuwa kila meli ya
mafuta inayoingia iwe zabuni inayojitegemea.
“Kwa kufanya hivyo kutatoa fursa
kwa watanzania kuweza kuingiza mafuta kwa sababu itapunguza gharama na uzuri
utakuwa nchi itanufaika kuwa na watanzania wengi kushiriki katika kuingiza
mafuta,”alisema.
Aliongeza kuwa kupita utaratibu
mpya wanaamini kuwa makampuni ya Tanzania yatapata faida kubwa na TRA kukusanya
mapato mengi.

No comments:
Post a Comment